Cosmas Nshenye, Mkuu wa wilaya ya Mbinga. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye ametoa
amri kwa Makampuni yanayonunua kahawa wilayani humo kuhakikisha kwamba ndani ya
siku 14 kuanzia sasa, yawe yamekamilisha malipo ya awamu ya pili ya fedha za
wakulima wa kahawa na kwamba kampuni itakayoshindwa kutekeleza amri hiyo
itachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.
Aidha ametoa agizo kwa wafanyabiashara wote
wanaojishughulisha na biashara ya zao hilo, kuandaa takwimu za malipo na mauzo
ya kahawa ambapo mara baada ya msimu wa mauzo kwisha, takwimu hizo ziwasilishwe
ofisini kwake ili serikali iweze kuzifanyia kazi.
Nshenye alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza kwenye
kikao cha Wadau wa kahawa wilayani hapa, ambacho kilishirikisha
wafanyabiashara, vikundi vya wakulima na makampuni ambayo hujishughulisha na
ununuzi wa zao hilo wilayani humo.
“Ndugu zangu hili sio ombi, takwimu hizi tukishazipata zitaisaidia
serikali kutambua ni nani ameuza kahawa hasa kwa wale watu wajanja wasiokuwa na
mashamba, ambao hupita vijijini kwa wakulima na kuendelea kumnyonya mkulima abaki
kuwa maskini’, alisema Nshenye.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Nshenye alisisitiza kuwa ni
marufuku kwa mfanyabiashara yeyote kupita majumbani kwa mkulima na kununua
kahawa badala yake watumie vituo maalumu vilivyowekwa na serikali, kwa ajili ya
kununulia zao hilo.
Alisema kuwa haitaji kuona mtu au kampuni inakiuka taratibu
na sheria zilizowekwa na serikali na kwamba kwa atakayeona masharti yaliyowekwa
hawezi kuyafuata, ajiondoe mapema kabla mkono wa sheria haujamfikia na kujikuta
yupo mahali pabaya.
Vilevile aliiagiza Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Kanda ya
Ruvuma, kuhakikisha kwamba inafuatilia mikataba yote ya makampuni yanayofanyabiashara
ya kahawa wilayani humo na mkulima, ili kujiridhisha kama mikataba hiyo
inamsaidia mkulima huyo na ofisi yake ipewe majibu ndani ya siku 14 kuanzia
sasa.
Hata hivyo aliongeza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuweza
kubaini mikataba yote yenye utata ambayo haimsaidii mkulima, ili serikali iweze
kuingilia kati na kuchukua hatua husika ya kurejesha haki zote za mkulima
ikiwemo kampuni au mfanyabiashara husika kuwajibishwa kwa kufutiwa leseni yake
ya biashara ya kahawa.
No comments:
Post a Comment