Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge amewataka Wadau
mbalimbali katika mkoa huo kuona umuhimu wa kuendelea kushirikiana na Serikali
katika shughuli za maendeleo ya wananchi, ili kuweza kuharakisha ukuaji wa
uchumi ndani ya mkoa huo.
Dkt. Mahenge alitoa kauli hiyo juzi mjini Namtumbo mkoani
hapa, wakati alipokuwa akifungua kikao maalumu kwa ajili ya uanzishaji wa Benki
ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma, kilichofanyika mjini hapa.
Alisema kuwa kuazishwa kwa benki hiyo ni agizo lililotolewa
na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, katika kikao chake na Wakuu wa mikoa mjini
Dodoma kwamba kila mkoa unapaswa kuona umuhimu wa kuanzisha benki ya
wananchi ili iweze kusaidia kukua kwa uchumi na kusogeza huduma za kifedha kwa
karibu zaidi katika eneo husika.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa kupitia fursa hiyo, kipato cha
mwananchi mmoja mmoja kitaongezeka kutoka wastani wa shilingi milioni 2,082,167
kwa takwimu za mwaka 2014 hadi kufikia wastani wa shilingi milioni
3,257,368 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Alisema zaidi ya asilimia 90 ya uchumi wa mkoa wa
Ruvuma, unategemea kilimo kwani mkoa huo ni miongoni mwa mikoa michache yenye
uzalishaji mkubwa wa mazao ya aina mbalimbali ya chakula na biashara, ambapo
uzalishaji wake hutegemea kwa kiasi kikubwa nguvu ya mwananchi mmoja mmoja
ambapo serikali imekuwa ikisaidia kutoa pembejeo za kilimo kwa mfumo wa ruzuku
kwa mazao ya nafaka.
Licha ya mafanikio hayo aliongeza kuwa bado wakulima wa mkoa
huo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile kukosa mitaji ya
kuendeshea shughuli zao za kilimo, ambapo hali hiyo inasababishwa na masharti
magumu ya mikopo itolewayo na taasisi za kifedha na kwamba hivi sasa hapa
Ruvuma kuna benki moja tu ya wananchi iliyopo katika wilaya ya Mbinga mkoani
humo, ambayo huwasaidia wakulima katika kuinua sekta ya kilimo kwa kuzalisha
mazao ya chakula na biashara, ambayo ni Mbinga Community Bank (MCB).
Kwa mujibu wa Dkt. Mahenge alieleza kuwa benki hiyo ndiyo
imekuwa ikiwasaidia wakulima wengi kupata mikopo, yenye gharama nafuu ya
pembejeo za kilimo na shughuli nyingine za ujasiriamali katika kuendesha maisha
yao.
No comments:
Post a Comment