Na Muhidin Amri,
Tunduru.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma,
kimeishukuru serikali kwa kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa barabara kwa
kiwango cha lami kwa wananchi wa wilaya hiyo na ukanda wote wa mikoa ya nyanda
za juu Kusini.
Chama hicho kimesema kwamba kukamilika kwa ujenzi wa barabara
hiyo kutoka Songea hadi wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, kupitia Tunduru
ambayo ilikuwa na mateso makubwa kwa wananchi kutokana na kupitika kwa shida
nyakati za masika hivi sasa ujenzi huo utasaidia kufungua fursa za kiuchumi, mawasiliano
na hata kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Hayo yalisemwa jana mjini hapa na Katibu wa CCM wa
wilaya hiyo Mohamed Lawa wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake juu ya hatua ambazo serikali ya awamu ya tano imeanza kutekeleza kwa
wananchi wa wilaya ya Tunduru.
Lawa alisema kuwa mbali na ujenzi wa barabara hiyo pia
serikali imekamilisha mradi wa ujenzi wa njia kuu za kusambaza nishati ya
umeme katika vijiji 19 jimbo la Tunduru Kaskazini ambapo mradi huo unaendelea kujengwa
kwa vijiji vyote vilivyopo pia katika jimbo la Tunduru Kusini, hivyo kuanza
kuleta matumaini kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Alifafanua kuwa kukamilika kwa mradi wa barabara hiyo kumesaidia
kuongezeka kwa shughuli za utalii kwani hata Watalii wengi kutoka nje na ndani
ya mkoa wa Ruvuma, wameanza kwenda kwa wingi hasa ikizingatia kuwa wilaya hiyo
imezungukwa na hifadhi ya taifa ya Selou, ambapo wananchi wanatakiwa kutumia
fursa hiyo kujenga nyumba na hoteli za kisasa kwa ajili ya kukuza uchumi wao.
“Kutokana na kufunguka kwa barabara hii ni matumaini yetu watu
wengi zaidi watafika hapa wilayani kwa ajili ya shughuli mbalimbali, hivyo
tunawataka wananchi kuongeza uzalishaji wa chakula mashambani na kujiepusha
kuuza ardhi yao hovyo kwa wageni badala yake wawekeze kwa faida ya kizazi cha
sasa na baadaye”, alisema Lawa.
No comments:
Post a Comment