Na Muhidin Amri,
Songea.
MANISPAA ya Songea mkoani Ruvuma, inatarajia kutumia zaidi ya
shilingi milioni 448 kwa ajili ya kufanya kazi ya ujenzi wa mradi wa maji katika
mtaa wa Ruhuwiko kanisani ili kuweza kuwaondolea kero wananchi ya ukosefu wa
maji, ambayo imedumu kwa muda mrefu sasa.
Samwel Sanya ambaye ni Mhandisi wa maji katika Manispaa hiyo,
alimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa tayari wamekwisha ingia mkataba na
mkandarasi wa Kampuni ya Giraf Investment, kwa ajili ya kuanza kazi ya ujenzi
huo.
Alifafanua kuwa upembuzi yakinifu kwa mradi huo, umefikia
asilimia 95 ambapo ulifanywa mwaka wa fedha wa 2012/2013 na kwamba ujenzi wake
hivi sasa ambao unaendelea kutekelezwa, umefadhiliwa na benki ya dunia.
Sanya alieleza kuwa mkandarasi huyo hadi sasa amelipwa zaidi
ya shilingi milioni 307 na kiasi ambacho bado anaidai Manispaa hiyo, ni zaidi
ya shilingi milioni 181 hivyo atamaliziwa kulipwa mara baada ya kazi husika
kukamilika kwake.
“Mradi huu bado haujakabidhiwa kwa wananchi, bado mkandarasi
anatudai tunachosubiri hapa ni kukamilisha malipo ya mkandarasi huyu ili tuweze
kuwakabidhi wananchi hawa”, alisema.
Alibainisha kuwa mradi huo unatumia nguvu ya umeme kupandisha
maji kwenye tanki kubwa lililojengwa, hivyo watumiaji wa maji watatakiwa hapo
baadaye kuchangia gharama kidogo ambazo zitasaidia kufanyia ukarabati pale
patakapokuwa na hitilafu za kawaida.
Mbali na hilo lengo la idara hiyo pia ni kuukabidhi mradi huo,
kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) ambao ndiyo watasimamia
uendeshaji wake ili uweze kuwa endelevu.
Wakati huo huo Manispaa ya Songea, imekamilisha pia ukarabati
wa visima viwili vya maji ambavyo vinatarajia kuhudumia watu zaidi ya 500.
Mhandisi Sanya amevitaja visima hivyo kuwa ni kile kilichopo
katika shule ya sekondari Mdandamo kata ya Mletele mjini hapa, ambacho
kimegharimu shilingi milioni 2.2 na kisima kingine cha shule ya msingi
Luhira kata ya Mshangano ambacho kimegharimu shilingi milioni 2.8.
No comments:
Post a Comment