Na Kassian Nyandindi,
Tunduru.
MAAFISA Watendaji wa kata katika
halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wametakiwa kuhakikisha kwamba
zoezi la kufyatua tofari kwa kila kijiji wilayani humo linatakiwa liwe
limekamilika mapema iwezekanavyo Septemba 15 mwaka huu.
Aidha wamesisitizwa kusimamia
ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao ya utendaji kazi, ambapo kila mnunuzi wa
mazao mchanganyiko anatakiwa kuwa na kibali cha ununuzi kutoka halmashauri ya
wilaya hiyo na leseni hai ya biashara husika.
Agizo hilo lilitolewa na Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Abdallah Mussa alipokuwa katika
kikao cha kazi juzi akizungumza na Watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo
mjini hapa.
Pia Mussa alipiga marufuku kwa
wanunuzi wa mazao hayo kutumia mizani ya saa kutokana na udanganyifu mkubwa unaofanywa
na baadhi ya wanunuzi kwa kuweka vitu vinavyoongeza uzito kama vile mchanga,
misumari na sumaku hivyo kuwaibia wakulima.
“Tutazunguka kila kijiji, kata, mtaa
na vitongoji vyote vilivyopo hapa wilayani nikikuta mnunuzi anatumia mizani ya
saa mtendaji kazi hakuna, sitaki kuona mtumishi katika wilaya hii anazembea
katika majukumu yake ya kazi”, alisisitiza Mussa.
Hata hivyo watendaji hao amewapatia
muda wa wiki mbili, waainishe maghala yote mabovu kupitia viongozi wa vijiji
ili halmashauri ya wilaya ya Tunduru iweze kupata taarifa ya tathimini ya
pamoja ni jinsi gani nguvu ya wananchi inaweza kutumika, katika kukarabati
maghala hayo ambayo ni chakavu.
No comments:
Post a Comment