Thursday, September 15, 2016

WATAKIWA KUTUMIA UTAJIRI WALIONAO KUPELEKA WATOTO WAO SHULE

Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

WAZAZI na Walezi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wametakiwa kutumia utajiri walionao wa kilimo cha zao la kahawa wilayani humo, kwa kuwapeleka watoto wao shule kwani ndiyo msingi mzuri wa maisha yao ya sasa na baadaye badala ya  kuwarithisha mali walizonazo.

Aidha hakuna ufahari kuwarithisha watoto mali au mashamba, kwani yanaweza yasiwasaidie maishani mwao na kuwafanya washindwe kusonga mbele kimaendeleo kutokana na kukosa elimu itakayowasaidia waweze kuondokana na adui ujinga, maradhi na umaskini.

Ofisa elimu msingi wa wilaya ya Mbinga, Samwel Komba alitoa rai hiyo juzi alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ruanda kata ya Ruanda  wilayani humo juu ya umuhimu wa kuchangamkia fursa ya mpango wa upimaji ardhi, kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na suala zima la kuwapatia watoto wao elimu bora ili iweze kuwasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maisha yao.


Pia Komba aliwataka wakazi wa kijiji hicho kujiandaa kuupokea mpango huo wa upimaji ardhi yakiwemo mashamba na maeneo ya makazi yao unaoratibiwa na halmashauri ya wilaya hiyo, kutokana na umuhimu wake kiuchumi kwa kuwa wananchi wenye maeneo yaliyopimwa watapata hati miliki ambazo zitatumika kwa ajili ya shughuli nyingine za kukuza uchumi wao.

Alisema kuwa katika kijiji cha Ruanda na  vijiji vingine vinavyozunguka kata hiyo vimekuwa na mabadiliko makubwa katika suala zima la kimaendeleo, kwani hivi sasa kutokana na uwepo wa shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe kuna wageni wengi wanaowasili huko kwa ajili ya shughuli mbalimbali, hivyo kuna kila sababu ya wao kuupokea mpango huo ili kuweza kuongeza thamani ya ardhi yao na waweze hata kuiuza kwa bei kubwa.

“Ndugu zangu naomba niwaelezeni mpango huu una faida nyingi kwenu, pimeni ardhi yenu ili mpate hati miliki zitakazoweza kuongeza thamani ya vipande vyenu vya ardhi mlivyonavyo, ili hata kama kuna mgeni anakuja kwenu kutaka kuinunua utaweza kuuza kwa bei nzuri”, alisema Komba.


Kadhalika aliwahakikishia wananchi hao kuwa mpango wa upimaji ardhi umekuwa mkombozi mkubwa kwa watu wengi maskini katika mikoa mbalimbali hapa nchini, kwani mbali ya kupata hati miliki pia wataweza kutumia hati hizo kukopa fedha katika taasisi za kifedha na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

No comments: