Na Kassian Nyandindi,
Songea.
AGIZO limetolewa kwa Watendaji wote wa Halmashauri za wilaya
ya Songea mkoani Ruvuma, kuhakikisha kwamba wanawapiga faini wananchi ambao wataonekana
kutotii amri ya kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ili iweze kuwa
fundisho kwa wengine na kuleta mabadiliko chanya, kwa jamii kujenga tabia ya
kufanya usafi katika maeneo yao.
Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema alitoa agizo hilo
juzi wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa mtaa wa Miembeni kata ya Bombambili
mjini hapa, ambako shughuli za usafi wa mazingira kiwilaya zilikuwa zikifanyika
na kuongozwa naye.
Kwa ujumla wilaya hiyo inaundwa na halmashauri tatu ambazo ni
Manispaa ya Songea, halmashauri ya wilaya ya Songea na ile ya Madaba.
Mgema alisema kuwa watu wote ambao hawataki kufanya usafi wa
mazingira kuanzia sasa watozwe faini ya shilingi 50,000 na kwamba anataka
ripoti ya watu hao pale wanapotozwa ifikishwe ofisini kwake haraka, ili aweze
kutambua ni nani wenye tabia ya kugoma kufanya usafi ili waweze kuchukuliwa
hatua zaidi.
Alifafanua kuwa taarifa alizonazo ni kwamba, kuna baadhi ya
wakazi waliopo katika mitaa mbalimbali ndani ya wilaya hizo wakiwemo pia wafanyabiashara
wamekuwa na mazoea ya kugoma kujitokeza kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho
wa mwezi, hali ambayo inawakatisha tamaa wengine wenye moyo wa kutekeleza jambo
hilo muhimu.
“Natoa agizo kwa Ofisa afya wa halmashauri ya Manispaa Songea
na timu yote ya ya uongozi wa kata na mitaa, hakikisheni wale wote ambao hawashiriki
kufanya usafi wanakamatwa na kupigwa faini ya shilingi 50,000 kila mmoja”,
alisisitiza Mgema.
Kadhalika aliongeza kuwa, jukumu la kufanya usafi ni la kila
mmoja ili kuweza kuepukana na magonjwa yanayotokana na uchafu kutokana na
mazingira kuwa na hali mbaya ya uchafu.
Vilevile kwa upande wake Ofisa afya wa Manispaa hiyo, Maxensius
Mahundi alimhakikishia Mkuu
huyo wa wilaya ya Songea kwamba idara yake imejipanga kikamilifu katika kusimamia
masuala ya usafi wa mazingira kwa vitendo na kwamba, tayari wamenunua magari
matatu ya kuzolea taka ambayo yatasaidia kupunguza kero ya kuzoa taka
zitakazolundikana katika maghuba.
Mahundi aliongeza kuwa katika kukabiliana na watu wanaochafua
mazingira kila kata itatoa vijana kumi, ambao watapewa mafunzo juu ya kusimamia
masuala ya usafi kwenye mitaa na kata zao.
No comments:
Post a Comment