Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
imetenga mbegu tani sita za zao la mbaazi kwa wakulima wa wilaya hiyo sawa na
kilo 6,000 kwa lengo la kuwataka wakulima hao, kufufua zao hilo ili waweze
kuinua uchumi wao na kuacha kutegemea zaidi zao la kahawa na mahindi.
Kwa mujibu wa Ofisa kilimo wa wilaya hiyo, Yohanes Nyoni
alisema kuwa kilo hizo 6,000 zitapandwa katika ekari 2,000 ambapo kila ekari
moja itapandwa kilo tatu za mbegu za mbaazi na kwamba zitasambazwa katika
maeneo yanayostawi vizuri ili wakulima waanze kuzalisha katika msimu ujao wa 2016/2017.
Nyoni alisema kuwa usambazaji wa mbegu hizo kwa wakulima
wilayani Mbinga ni mkakati pia wa kuboresha na kuongeza vyanzo vya mapato, hususani
kwenye mazao ya chakula na biashara yanayozalishwa wilayani humo.
“Tukizalisha mazao mengi ya aina mbalimbali hapa kwetu, hasa
kwa mazao haya ya chakula na biashara tutaiwezesha halmashauri yetu kupata
fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi
wetu”, alisema Nyoni.
Ofisa kilimo huyo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa katika kuhakikisha
kwamba zao la mbaazi linaleta tija na kusaidia kukua kwa uchumi wa wilaya
pamoja na kubadili maisha ya wananchi wake, halmashauri hiyo kupitia idara yake
ya kilimo imekwisha fanya utafiti kwamba ni maeneo gani
yanayostawi vizuri zao hilo ili kuweza kupata mavuno mengi.
Alisisitiza kuwa wakulima hupewa mafunzo ya kuzalisha mbaazi
kwa kufuata kanuni za kilimo bora na kwamba, endapo mkulima atazingatia kanuni
hizo ekari moja anao uwezo wa kuvuna gunia nane hadi 10.
“Gunia moja huwa na uzito wa kilo 90 ambapo kilo moja ya
mbaazi huuzwa kwa shilingi 3,500 hadi 4,000 kulingana na hali ya soko, hivyo
tunawashauri wakulima wetu wazalishe kwa wingi ili waweze kuwa na kipato
zaidi”, alisema.
Pamoja na mambo mengine aliongeza kuwa mbali na halmashauri ya
wilaya ya Mbinga kuwapatia wakulima hao mbegu hizo, pia itatoa pembejeo za
kilimo ikiwemo madawa na mbolea pamoja na kuwatafutia soko la uhakika kwa ajili
ya kuuza mazao yao.
Katika hatua nyingine Nyoni amewaonya wanunuzi wa mazao ya
chakula na biashara wanaokwenda wilayani humo, kufuata taratibu zilizopo ikiwemo
kununua mazao katika vituo maalumu vilivyotengwa na halmashauri na sio kwenda
moja kwa moja shambani kwa mkulima kwani kitendo hicho kimekuwa kikisababisha
kuwanyonya na kuwatia hasara wakulima.
No comments:
Post a Comment