Sunday, February 26, 2017

MWALIMU SHULE YA SEKONDARI KIAMILI MBINGA ATAFUTWA NA POLISI KWA KUMSHAMBULIA MWANDISHI WA HABARI

Na Mwandishi wetu,      
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamtafuta Mwalimu wa shule ya sekondari Kiamili wilaya ya Mbinga mkoani humo, Victor John Kayombo ambaye amekimbia hajulikani wapi alipo kwa kosa la kumshambulia mwandishi wa habari, kumpiga na kutaka kumjeruhi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizomfikia mwandishi wa habari hizi zinaeleza kwamba tukio hilo lilitokea Februari 24 mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni katika mtaa wa Soko kuu Mbinga mjini.

Imefafanuliwa kuwa Kayombo alimshambulia mwandishi wa habari Kassian Nyandindi wa gazeti la Majira mkoani hapa, baada ya kumhoji masuala ya utoro kazini ambapo amekuwa akilalamikiwa kwa muda mrefu na Walimu wenzake wa sekondari hiyo kwamba, haudhurii ipasavyo vipindi vyake vya masomo darasani pale anapotakiwa kufundisha wanafunzi wa shule hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji.

Aidha imeelezwa kuwa tokea mwalimu huyo ahamie shuleni hapo Januari 11 mwaka 2016 akitokea shule ya sekondari Dokta Shein, iliyopo katika kata ya Mpepai halmashauri ya mji wa Mbinga amekuwa na tabia hiyo ya kutozingatia vipindi vya kufundisha watoto darasani.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mwalimu Kayombo amefunguliwa shauri hilo katika Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga, Jalada la uchunguzi lenye namba MBI/IR/286/2017 na baadaye aweze kufikishwa Mahakamani kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.

Awali kwa upande wake Nyandindi alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya hali hiyo alikiri kushambuliwa na mwalimu huyo ambapo alieleza kuwa ilitokana na kumhoji kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa Walimu wenzake shule ya sekondari Kiamili kwamba, haudhurii ipasavyo darasani hivyo walimu wenzake hulazimika kujitolea kufundisha masomo ambayo alipaswa yeye kuyafundisha shuleni hapo.


“Kwa mujibu wa taarifa za uhakika nilizonazo na mahudhurio ya mwalimu huyu ni kwamba ndani ya wiki moja huwa anawasili shuleni hapo mara mbili au mara moja kwa wiki, hii ni kwa mujibu wa taarifa za mahudhurio ya walimu wenzake ambazo ninazo”, alisema Nyandindi.

Vilevile Mkuu wa shule hiyo, Cornel Lwiwa alipohojiwa alithibitisha tatizo la kutohudhuria shuleni hapo mwalimu huyo na kuongeza kuwa taarifa zake zimeripotiwa ngazi mbalimbali za uongozi wa wilaya na mkoa.

“Tatizo la huyu mwalimu wangu kutohudhuria hapa shuleni kwa kweli ni kubwa sana, amekuwa wakati mwingine akitoka hapa shuleni bila ruhusa na hata mpaka sasa sielewi yupo wapi na hivi sasa nafikiria kwenda kwa afisa elimu sekondari ili achukue hatua za kisheria au abadilishiwe kituo cha kazi, kwa sababu sisi kama kituo kwa shule yangu tunapata hasara kubwa kutokuwepo kwake na kushiriki kikamilifu katika vipindi vya masomo darasani”, alisema Lwiwa.

Lwiwa alifafanua kuwa Kayombo amekuwa akifundisha somo la Kiswahili kwa wanafunzi wa kidato cha pili katika mikondo mitatu A, B na C na kwamba wanafunzi hao wakati mwingine wamekuwa wakikaa kwa muda wa wiki nzima hawasomi somo hilo kutokana na kuwa mtoro kazini.

Alibainisha kuwa hata katika kipindi cha Mwezi Januari mwaka huu wanafunzi walikuwa wakifanya mazoezi ya mtihani wa kila mwezi, lakini cha kushangaza mtihani wa somo la Kiswahili hadi leo hii ambao waliufanya wanafunzi hao karatasi zao walizofanyia hawajapewa na hawajui zipo wapi.


Hata hivyo kufuatia kuwepo kwa hali hiyo Ofisa elimu sekondari wa wilaya ya Mbinga, Joseph Kapere alithibitisha kuwepo kwa malalamiko hayo na kueleza kuwa taratibu husika zitafuata dhidi ya mtumishi huyo ikiwemo kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu.

No comments: