Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa ucheleweshaji wa utoaji haki kwa wakati unasababisha kupoteza rasilimali muda na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi,
hivyo wito umetolewa kwa wadau wote washeria kuhakikisha kwamba wanatenda haki
na kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas
Nshenye wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya sheria
nchini yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya Mahakama ya wilaya hiyo mjini
hapa.
“Nasisitiza kwamba zile kesi ambazo zinauwezekano wa kutolewa
dhamana zitolewe dhamana kwa wakati, tuache tabia ya kuwaweka mahabusu gerezani
tupunguze wasiwepo wengi wanaokaa huko bila sababu yoyote ile ya msingi”,
alisema Nshenye.
Alisema kuwa kuadhimisha siku ya sheria hapa nchini, kunaashiria
kuanza rasmi kwa shughuli za kimahakama hivyo kauli mbiu ya umuhimu wa utoaji haki kwa wakati kuwezesha
ukuaji wa uchumi, inapaswa kuzingatiwa kwa wadau wa sheria kufuata taratibu
na sheria zilizowekwa bila kujenga ukandamizaji au ubaguzi katika jamii.
Naye kwa upande wake Hakimu mkazi wa Mahakama ya wilaya ya
Mbinga, Magdalena Ntandu akitoa hotuba mbele ya wananchi waliohudhuria
maadhimisho hayo alisema kuwa upatikanaji wa haki kwa wakati kunasaidia jamii
kujenga imani kwa vyombo vyote vya utoaji haki, kutambua na kuheshimu uwepo wa
utawala wa sheria hapa nchini.
Ntandu alisema kuwa nchi yenye mfumo mzuri wa utawala wa
sheria inatoa pia fursa sawa kwa wananchi wake mbele ya sheria na kujenga jamii
yenye usawa, utulivu, ulinzi na amani.
“Na sio hivyo tu, hata pale haki inayotafutwa inapokuwa ni
mojawapo ya rasilimali muhimu katika kuendeleza ama kukuza uchumi, haki hiyo
ikicheleweshwa moja kwa moja inarudisha nyuma ukuaji wa uchumi wa mtu
anayetafuta haki hiyo”, alisema.
Alibainisha kuwa wajibu wa Mahakama na wadau wengine katika
utoaji haki kwa wakati, wanapaswa kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba
mashauri yote yaliyofunguliwa inapofikia mwishoni mwa mwaka yawe yamemalizika
ili unapoanza mwaka mwingine waweze kuanza na mashauri mapya.
Alifafanua kuwa kwa kutekeleza kauli mbiu ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania John Magufuli ya Hapa kazi tu, ina maana kwamba watu
wote wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na kuepuka visingizio visivyokuwa vya
lazima ambavyo vinakwamisha uadilifu na uwajibikaji ipasavyo katika jamii.
Pamoja na mambo mengine, awali naye Frank Kapinga
akiwakilisha mawakili wenzake kwa kutoa hotuba katika sherehe hizo za
maadhimisho ya siku ya sheria hapa nchini wilayani Mbinga, alifafanua kuwa zipo
sababu nyingi zinazokwamisha utoaji haki kwa wakati huku akizitaja baadhi yake
kuwa ni ukosefu wa miundombinu rafiki kwa utoaji haki, uhaba wa rasilimali
watu, mbinu na kanuni za kisheria za ucheleweshaji zinazoletwa na wadau wa
sheria wakiwemo serikali, mahakama, mawakili, na waendesha mashtaka.
Kapinga alisema kuwa Mahakama ikiwa ndiyo mhimili mkuu wa
utoaji haki inao wajibu ambao imepewa kikatiba, inapaswa kusikiliza na kumaliza
mashauri mbalimbali kwa muda unaostahili na kuondokana na tabia ya kuchelewesha
kesi kwa kuziahirisha pasipo hata sababu zenye mashiko.
“Mahakama inalojukumu la kupambana na vitendo hivi vinavyokiuka
maadili ya utendaji kazi hususani rushwa na jeuri ya madaraka ya kimahakama,
inapaswa kuhakikisha wadau wote wanapata huduma stahili na ushirikiano ili
waweze kutimiza majukumu yao ya kila siku kwa wakati”, alisisitiza Kapinga.
No comments:
Post a Comment