Na Kassian Nyandindi,
Songea.
HATIMAYE Watumishi saba wanaotoka katika Halmashauri ya mji
wa Mbinga, wilaya ya Mbinga na Nyasa mkoani Ruvuma ambao pia ni Wajumbe wa bodi
ya Chama cha ushirika Mbinga Kurugenzi SACCOS, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama
ya Hakimu mkazi mkoani humo wakituhumiwa kula njama na kutenda kosa la
kujipatia mkopo wa shilingi milioni 500 kutoka benki ya CRDB kinyume na
taratibu husika.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa Mahakamani hapo na
Mwendesha mashtaka ambaye ni Wakili wa serikali mkoani hapa, Shaban Mwegole
mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama hiyo Simon Kobero alidai kuwa
washtakiwa hao pia wanakabiliwa na makosa kumi, wakidaiwa kughushi nyaraka mbalimbali
na kufanikiwa kufanya wizi katika sehemu ya fedha hizo jambo ambalo limesababisha
hasara kubwa kwa chama hicho kushindwa kujiendesha kwa manufaa ya wanachama.
Mwendesha mashtaka huyo aliwataja washtakiwa wanaokabiliwa
kufanya makosa hayo na kufunguliwa kesi Jinai namba 1 ya mwaka 2017 kuwa ni,
Emmanuel Mwasaga, Alex Kalilo na Zackaria Lingowe ambao ni watumishi wa
halmashauri ya wilaya ya Nyasa, Jamima Challe na Stella Mhagama wanatoka
halmashauri ya mji wa Mbinga, Lucas Nchimbi na Mhadisa Meshack nao ni watumishi
wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga.
Aidha Mwegole aliendelea kudai Mahakamani hapo kuwa shtaka la
Kwanza linamkabili Emmanuel Mwasaga akiwa Mwenyekiti wa bodi ya ushirika huo
anadaiwa kwamba Novemba 7 mwaka 2015, alitumia mbinu za kuweza kupata mkopo huo
kwa kutoa cheti cha udanganyifu cha SACCOS hiyo chenye kuonyesha ukomo wa
madeni ili waweze kupewa fedha hizo kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi.
Mwegole alisema kuwa Mwasaga kwa kushirikiana na Wajumbe
wenzake wa bodi wanakabiliwa na kosa la pili ambapo katika mwaka huo, walitumia
muhtasari wa Novemba 23 mwaka 2015 wa vikao vya bodi kughushi nyaraka na kuweza
kujipatia mkopo huo kinyume na sheria za ushirika.
Vilevile alisema kuwa shtaka la tatu ni kwamba Wajumbe hao wa
bodi wanadaiwa kuiba fedha za chama hicho cha ushirika shilingi milioni
137,236,250 katika kipindi hicho cha Novemba 7 mwaka 2015 baada ya kufanikiwa
kujipatia mkopo huo kutoka benki ya CRDB.
Shtaka la nne mnamo mwaka 2014 hadi 2015 kwa nyakati tofauti
walitenda kosa la wizi wa uaminifu, wakiwa wote saba Wajumbe wa bodi hiyo
waliiba tena shilingi milioni 65 za Mbinga Kurugenzi SACCOS na kujinufaisha wao
binafsi.
Katika shtaka la tano Mwasaga akiwa Mwenyekiti wa bodi
anatuhumiwa pia kuiba shilingi milioni 3,931,124 kutoka katika SACCOS hiyo,
ambazo alikopeshwa kwa kuaminiwa kama mkopo ili baadaye aweze kulipa kupitia
mshahara wake jambo ambalo hajalitekeleza mpaka sasa.
Mwendesha mashtaka huyo alisema kwamba katika shtaka la sita,
alimtaja Alex Kalilo akiwa mjumbe wa bodi naye anadaiwa kuiba shilingi milioni
3,813,541 na shtaka la saba Mhadisa Meshack akiwa naye mjumbe wa bodi hiyo
aliiba shilingi milioni 1,615,000 fedha ambazo waliaminiwa kama mkopo ili
waweze kukatwa kupitia mshahara wao.
Pia Mwanasheria huyo wa serikali Mwegole aliongeza kuwa
katika kosa la nane shilingi milioni 5,550,000 zilichotwa na Stella Mhagama,
ambapo katika shtaka la tisa shilingi milioni 107,500,000 ziliibwa na Jamima
Challe huku shtaka la kumi shilingi milioni 9,835,000 ziliibwa na Lucas
Nchimbi.
Hata hivyo kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Februari 8 mwaka
huu kutokana na upelelezi bado haujakamilika ambapo washtakiwa wote kwa pamoja
walikana mashtaka, wapo nje kwa dhamana ya wadhamini wawili waaminifu kila
mmoja kwa shilingi milioni 25 na hati za mali zisizohamishika zenye thamani ya
shilingi milioni 50.
No comments:
Post a Comment