Na Mwandishi wetu,
Songea.
WAFUASI watatu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamepandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Hakimu mkazi mkoani humo, kwa tuhuma ya kula njama na kuharibu gari
la Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kulipiga mawe.
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali kanda
ya Songea Tumaini Ngiruka aliwataja Mahakamani hapo washitakiwa hao kuwa ni Joseph
Fuime (52) mkazi wa Songea mjini aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani
humo, Emmanuel Kalisinjesi (37) mkazi wa mtaa wa Ruvuma na Sedrick Komba (51) mkazi
wa Bombambili mjini hapa.
Mwendesha mashtaka ambaye ni Mwanasheria huyo wa Serikali kanda
ya Songea, Ngiruka alidai mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya mkoa
wa Ruvuma, Issa Magori kuwa mnamo Januari 20 mwaka huu majira ya usiku katika
eneo la mtaa wa Pambazuko uliopo nje kidogo ya Manispaa ya Songea washtakiwa hao
waliharibu gari la CCM aina ya Landcruiser lenye namba za usajili T 640 BEU kwa
kulipiga mawe na kusababisha kuvunjika kioo cha mbele ya gari hilo na upande wa
dereva.
Ngiruka aliendelea kudai Mahakamani hapo kuwa uhalifu huo
waliokuwa wameufanya watuhumiwa hao, walikuwa wakijua kwamba kutenda kosa hilo
ni kuvunja sheria za nchi.
Alisema kuwa baada ya tukio hilo kulifanya washtakiwa wote
watatu walikimbia ambapo walikamatwa baadaye na kufunguliwa mashtaka hayo.
Pamoja na mambo mengine washitakiwa hao wamekana mashtaka hayo
yanayowakabili na kwamba wapo nje kwa dhamana ya wadhamini wawili waaminifu
kila mmoja, hadi Februari 17 mwaka huu shauri hilo litakapotajwa tena.
No comments:
Post a Comment