Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa malengo makuu ya mpango wa bajeti kwa Halmashauri
ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ni kuimarisha amani na utawala bora, kuboresha
huduma za kijamii, kukuza uchumi wa wilaya hiyo kwa lengo la kuboresha maisha
ya wananchi wake, sambamba na dira ya maendeleo ya taifa inayolenga Tanzania
kuwa nchi ya viwanda vya kati.
Aidha halmashauri hiyo inaendelea na jitihada za kuongeza
vyanzo vipya vya mapato ya ndani badala ya kutegemea zao la kahawa pekee ambalo
hivi sasa halikidhi mahitaji husika, ambapo jitihada zinafanyika za kutafuta
wawekezaji watakaoweza kutumia rasilimali zilizopo wilayani humo kama vile madini,
ardhi na misitu viweze kuingiza mapato zaidi.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito wakati alipokuwa akitoa maelezo mafupi juu ya
rasimu ya mpango wa bajeti kwa Baraza maalum la Madiwani wa halmashauri hiyo, mwaka
wa fedha 2017 hadi 2018 lililoketi leo kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.
Samandito alisema kuwa kuongezeka kwa fedha hizo za mapato
kutatokana pia na fedha za upimaji wa mashamba ya kahawa ambapo ekari moja
hupimwa kwa shilingi 100,000 na kwamba tayari mashamba 70,000 ya wananchi
wilayani humo yamepimwa na wahusika kupewa hati za kimila huku halmashauri
ikiweza kupata shilingi bilioni 7,000,000,000.
Kadhalika aliongeza kuwa tayari viwanja 125,000 vimepimwa
katika miji midogo mbalimbali iliyopo wilayani hapa ambavyo vinatarajia
kuiingizia halmashauri shilingi bilioni 2,500,000,000 ambapo utekelezaji huu ni
wa sera ya taifa ya ardhi na mpango wa pili wa maendeleo ya taifa wa miaka
mitano unaotaka kila kipande cha ardhi kipimwe hapa nchini.
Afisa mipango wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Onesmo
Mapunda akiwasilisha bajeti ya mpango huo wa fedha kwa Baraza hilo la Madiwani, alisema kuwa bajeti ambayo wanatarajia kuitumia
katika kipindi hicho ni ya shilingi bilioni 46,591,949,782 ambapo kati ya hizo
shilingi bilioni 27,394,490,248 ni mishahara ya wafanyakazi, shilingi bilioni
1,809,347,616 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Pia katika bajeti hiyo shilingi bilioni 7,830,382,900
zitatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi na kwamba mapato ya
ndani yamekadiriwa kukusanywa kufikia shilingi bilioni 9,557,729,018.
Bajeti hiyo ilipitishwa katika kikao hicho ambacho kilikuwa
kikiongozwa na Mwenyekiti wake, Ambrose Nchimbi na kuhudhuriwa na wakuu wa
idara pamoja na watendaji wa kata wa wilaya hiyo na kueleza kuwa imezingatia
makubaliano waliyoketi katika vikao vya kamati mbalimbali.
Nchimbi alisisitiza kuwa vipaumbele vya bajeti hiyo ni
kukamilisha miradi ya miaka ya nyuma ambayo ilikuwa bado haijakamilika ujenzi
wake, pamoja na kuongeza vyanzo vipya vya mapato ya ndani badala ya kutegemea
zao la kahawa pekee ambalo hivi sasa halikidhi mahitaji husika ya halmashauri.
Aliongeza kuwa bajeti hiyo pia imelenga kuboresha ujenzi wa
miundombinu ya elimu katika shule za msingi na sekondari, kuboresha huduma za
afya kwa kukamilisha ujenzi wa zahanati, kutengeneza madawati na viti kwa ajili
ya shule za msingi na sekondari, ujenzi wa nyumba za watumishi katika shule za
msingi na sekondari, kuboresha mtandao wa barabara za halmashauri, pamoja na
kuandaa mpango mkakati mpya wa maendeleo ya wananchi na halmashauri kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti huyo wa halmashauri ya wilaya ya
Mbinga, Nchimbi amewapongeza pia Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Samandito
na Afisa mipango Mapunda pamoja na timu nzima ya wataalamu kwa kuandaa vizuri
taarifa ya bajeti na mpango wa maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo, kwa mwaka
wa fedha wa 2017/2018 ambapo amedai kuwa endapo itapitishwa na Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania itaweza kuleta sura nzuri ya mafanikio makubwa kwenye upande
wa miradi ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment