Sunday, February 12, 2017

SITA WAJERUHIWA VIBAYA NA MMOJA AFARIKI DUNIA BAADA YA KUPIGWA NA RADI

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

WATU sita wanaoishi katika kitongoji cha Kifaguro kijiji cha Lituta wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wamejeruhiwa vibaya na mtu mmoja kufariki dunia baada ya kupigwa na radi kufuatia mvua kubwa ambayo iliambatana na upepo mkali, kuezua nyumba zenye kaya 37 na kusababisha kuharibika kwa mali mbalimbali zilizokuwemo ndani ya nyumba hizo.

Katika tukio hilo wakazi 79 wa kitongoji hicho pia wamekosa mahali pa kuishi ambapo habari zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 4 mwaka huu majira ya saa 9 alasiri.

Mwombeji alifafanua kuwa siku ya tukio hilo mvua hiyo iliambatana na upepo mkali na kusababisha kuezuliwa kwa nyumba hizo na vitu mbalimbali vilivyokuwemo ndani yake viliharibika ikiwemo vyakula ambapo thamani yake halisi bado haijajulikana.


Alieleza kuwa mvua hiyo pia ilisababisha watu sita kujeruhiwa vibaya katika maeneo mbalimbali ya miili yao ambao walipelekwa katika kituo cha afya Madaba kwa ajili ya kupatiwa matibabu na baadaye waliruhusiwa kurudi makwao ambapo aliwataja majeruhi hao kuwa ni Ernousi Nganena (24) aliyejeruhiwa vibaya kichwani pamoja na miguuni.

Wengine wametajwa kuwa ni Boni Lupungwe (28) aliyejeruhiwa kwenye maeneo ya magoti na kupata maumivu makali kwenye mbavu, Patrick Mhoha (34) aliyeangukiwa na matofari ya Nyumba yake katika mguu wa kulia, Kalistus Mtega (40) ambaye alipata jeraha kichwani na kuchubuka mguu wa kulia, Nicodemu Mhada (34) alipata michubuko miguuni na kuwa na maumivu makali kiunoni na Philemon Mbunda (29) aliyejeruhiwa katika paja lake la mguu wa kulia huku akiwa na maumivu sehemu mbalimbali za mwili wake.

Wakati huo huo, katika kitongoji cha Ifungwa kilichopo kijiji cha Madaba kata ya Mahanje wilaya ya Songea mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Hadson Mtitu (41) alifariki dunia baada ya kupigwa na radi ambayo ilisababisha pia majeraha kwa mke wake Sesilia Kisite (35).

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 4 mwaka huu majira ya saa 9:30 alasiri huko katika kitongoji hicho wilayani humo.

Alisema kuwa siku hiyo ya tukio Mtitu akiwa na mke wake Sesilia Kisite walikuwa wamejihifadhi kwenye kibanda kilichopo shambani kwao wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha ghafla radi ilipiga na kumsababishia Mtitu umauti papo hapo.


Hata hivyo alifafanua kuwa mke wa marehemu Mtitu hivi sasa anaendelea kupata matibabu katika kituo cha Afya Madaba na kwamba mwili wa marehemu huyo ulifanyiwa uchunguzi na askari waliofika kwenye eneo la tukio kwa kushirikiana na Mganga ambaye waliongozana naye na kuthibitisha kuwa Mtitu amefariki dunia.

No comments: