Samson Kahabuka, Mratibu wa kituo cha habari za utalii mkoa wa Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MASHINDANO ya kumtafuta Balozi wa utalii mkoa wa Ruvuma,
ambayo yanaratibiwa na Kituo cha habari za utalii mkoani humo yameanza kufanyika
kwenye hoteli ya Majimaji iliyopo mjini Songea.
Mratibu wa kituo hicho, Samson Kahabuka alisema kuwa warembo
15 kutoka wilaya ya Songea wameanza mazoezi kwenye ukumbi wa hoteli hiyo ambapo
lengo kuu la kufanya hivyo ni kuwapata warembo watakaotoka wilaya zote za mkoa huo.
Kahabuka alisema lengo kuu la shindano hilo ni kutangaza
vivutio vyote vya mkoa wa Ruvuma, ambapo Februari 10 mwaka huu warembo 15
kutoka wilaya ya Songea watatembelea wilaya ya Nyasa ili kuweza kuona baadhi ya
vivutio vya wilaya hiyo.
Pia alisema kuanzia wiki ya tatu ya mwezi Februari hadi Machi
mwaka huu, warembo hao watafanya ziara ya kutembelea vivutio vya utalii ambavyo
vipo mkoani hapa.
Mratibu huyo aliongeza kuwa fainali za kumpata Balozi huyo mkoani
Ruvuma zinatarajiwa kufanyika Machi 31 mwaka huu mjini Songea.
Hata hivyo Kahabuka aliyataja baadhi ya manufaa ambayo
mshiriki atayapata katika shindano hilo ni pamoja na kupata elimu ya mambo
mtambuka ikiwemo elimu ya kujitambua, fursa ya ajira kwenye hoteli na kwamba
kwa atakayeshinda atawakilisha mkoa huo ngazi ya kitaifa.
No comments:
Post a Comment