Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.
MWENYEKITI wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
Ambrose Nchimbi amewataka viongozi wa kisiasa na watendaji katika maeneo
mbalimbali wilayani humo, kujenga ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao na
kuacha kuendekeza malumbano badala yake wasimamie vyema ujenzi wa miradi ya
wananchi ili iweze kukamilika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.
Akizungumza na mwandishi wetu, Nchimbi alisema kuwa baadhi ya maeneo
wilayani humo miradi ya wananchi ya maendeleo imekwama haijakamilika kwa wakati
uliopangwa kutokana na tabia ya viongozi kuendekeza malumbano hasa
yanayochochewa na viongozi wa vyama vya siasa.
Alivinyoshea kidole vyama vya upinzani kutokana na tabia ya
viongozi wake kuwakatisha tamaa wananchi kwa kuwadanganya kuwa serikali
imewasahau kitu ambacho sio cha kweli.
Alifafanua kuwa Madiwani wa vyama hivyo wamekuwa mstari wa
mbele kuwadanganya wananchi, wakiwaelekeza kwamba kwenye maeneo yao wasichangie
nguvu zao katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo jambo ambalo alisema ni
upotoshaji ambapo halipaswi kuungwa mkono kwani kitendo hicho ni sawa na kuhamasisha
umaskini uendelee kuwepo miongoni mwa jamii.
Nchimbi alisema serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi za
utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri zake, lakini kama
viongozi hawataonesha ushirikiano mzuri upo uwezekano mkubwa wa kutotekelezeka
kwa miradi hiyo.
“Wakati umefika kwa viongozi wa ngazi zote kushirikiana na
kufanya kazi za kusimamia utekelezaji wa miradi hii ya maendeleo ambayo imeibuliwa
na wananchi ili iweze kukamilika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa”,
alisisitiza Nchimbi.
No comments:
Post a Comment