Sunday, February 12, 2017

WANAFUNZI AMBAO HAWAJARIPOTI SHULE KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

MAOFISA elimu katika Halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji na kata wametakiwa kuhakikisha kwamba watoto wote waliochaguliwa kwenda shule kwa ajili ya kuanza kidato cha kwanza wanaripoti haraka katika shule husika, kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.

Agizo hilo limetolewa juzi na Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alipokuwa akizungumza na Madiwani, Maofisa elimu na Watendaji wa halmashauri hizo mjini hapa huku akieleza kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari mwaka huu mpaka sasa kwa shule hizo za sekondari jumla ya wanafunzi 120 hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa kwenda kusoma wilayani humo, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuchukua hatua ili kuweza kudhibiti hali hiyo isiweze kuendelea kuwepo na kujenga mazoea katika jamii.

“Naendelea kusisitiza kwamba wanafunzi wote waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanapaswa kwenda shuleni kusoma, nawataka maofisa elimu na watendaji wa vijiji na kata mshirikiane kumaliza tatizo hili mapema na ofisi yangu ipate taarifa haraka kwamba watoto hawa wapo shuleni wanasoma”, alisisitiza.


Akizungumzia juu ya suala la watoto wa kike kupewa mimba, Nshenye alisema kuwa yeye peke yake hana uwezo wa kudhibiti tatizo hilo hivyo wananchi wanalojukumu la kujenga ushirikiano katika kukemea jambo hilo lisiendelee kuwepo na pale wanapobaini kuna tatizo, ni vyema hatua zichukuliwe haraka na wazazi waache tabia ya kumalizana mitaani huku mtoto wakimwacha akiwa na hali mbaya.

“Ndugu zangu kuhusiana na suala hili la mimba mimi kama Mkuu wa wilaya sina uwezo wa kudhibiti tatizo hili kwa watoto hawa wa kike tunapaswa tushirikiane kwa pamoja ili tuweze kupambana na jambo hili, tatizo hapa ipo shida kubwa wananchi wamekuwa na tabia ya kumalizana mitaani kwa kupeana mbuzi na ng’ombe kwa lengo la kuficha ukweli uliopo”, alisema Nshenye.

Kwa upande wao wakichangia hoja katika kikao hicho cha baraza la madiwani, diwani wa kata ya Mpepai Benedict Ngwenya alisema kuwa kuna kila sababu sasa kwa madiwani kuhamasisha wazazi katika kupambana na tatizo hilo ambalo linaonekana kutishia ustawi wa maendeleo ya elimu wilayani humo.

Ngwenya alisisitiza kuwa endapo suala hilo litafumbiwa macho kutakuwa na hatari kwa siku za mbele kuwa na kizazi kisichokuwa na elimu kutokana na kutosoma shule, hasa kwa watoto wa kike ambao wamekuwa wakipewa mimba na kesi zao haziripotiwi ipasavyo ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wahusika wanaofanya hivyo.

No comments: