Monday, February 13, 2017

AFISA KILIMO HALMASHAURI MJI WA MBINGA ADAIWA KUINGIA MITINI NA MBEGU ZA WAKULIMA WA TANGAWIZI

Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma.
Na Dustan Ndunguru,       
Mbinga.

MALALAMIKO yametolewa na baadhi ya Wananchi waishio katika kata ya Kihungu Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, dhidi ya Kaimu Ofisa kilimo wa halmashauri hiyo, Maganga Ngahy wakimshutumu kutokana na kitendo chake cha kuwapelekea mbegu pungufu za zao la Tangawizi wananchi wa kata hiyo, ambazo walipaswa kuzalisha katika mashamba yao katika msimu wa mwaka huu.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti Wanachama wa kikundi cha JITUME waliopo katika kata hiyo walisema kuwa kabla ya kupelekewa mbegu hizo walielezwa kwamba wangepata kilo 500 za zao hilo, lakini cha kushangaza wamepewa kilo 400 tu huku kukiwa na upungufu wa kilo 100 jambo ambalo limewafanya washindwe kutimiza ndoto yao ya kupanda eneo lote walilotarajia kupanda Tangawizi hizo.

Walisema kuwa mbegu hizo za Tangawizi wanachotambua ni kwamba wamekopeshwa ili wakati wa mavuno utakapowadia wanapaswa kurejesha baadhi ya mbegu kwa wakulima wengine, ambapo wasiwasi wao walionao sasa ni kwamba kutokana na kupatiwa mbegu pungufu watashindwa kurejesha kiasi husika ipasavyo ukizingatia kwamba uongozi wa halmashauri hiyo unatambua wao wamepewa kilo zote miatano na sio vinginevyo.


“Kwa kweli hili alilolifanya huyu Ofisa kilimo linatukatisha tamaa ya kuendelea na uzalishaji wa zao hili yeye alipaswa kutuletea kilo zote miatano ili wenzetu kwa siku zijazo waweze pia kunufaika na uzalishaji wa zao hili, wenzetu katika vikundi vingine tunazo taarifa kwamba wamepewa kilo zote miatano sijui kwa nini sisi tumedhulumiwa tunaziomba mamlaka husika ifanyie kazi jambo hili”, walisema.

Ofisa mtendaji wa kata ya Kihungu, Issack Ndunguru alithibitisha Wanachama wa kikundi hicho kupokea kilo 400 za Tangawizi badala ya kupewa kilo 500 ambazo zimekuwa zikitolewa kwa kila kikundi kilichopo katika kata hiyo kinachojishughulisha na uzalishaji wa zao hilo ili waweze kuzalisha kwenye mashamba yao.

Ndunguru alifafanua kuwa baada ya kuliona hilo alimfuata Kaimu Ofisa kilimo, Ngahy ambapo baada ya kumweleza suala hilo, alikiri kuwa kikundi hicho hakikupatiwa mbegu zote kama ilivyokusudiwa lakini hakueleza sababu za msingi kwa nini hawakupewa mbegu hizo kamilifu.

Kwa upande wake Ngahy alipofuatwa na mwandishi wetu alisema ni kweli wanachama wa kikundi hicho hawajapata mbegu zote, huku akishindwa kueleza ni lini watapata mbegu zao za Tangawizi ili waweze kupanda mapema kabla msimu wa mvua haujakwisha.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Robert Mageni alishangazwa na kitendo hicho kilichofanywa na mtumishi huyo ambapo alisisitiza kuwa atafuatilia suala hilo na kulipatia ufumbuzi mapema ikiwemo kumchukulia hatua dhidi ya aliyehusika na hujuma hiyo.

Mageni alisema kuwa serikali imekuwa ikielekeza kila halmashauri iwezeshe vikundi vya vijana na wanawake kwa kutenga asilimia kumi ya mapato yake ya ndani, hivyo kamwe halmashauri yake haiwezi kuwaendekeza watumishi ambao wanakwamisha kwa makusudi juhudi zinazofanywa na serikali kwa lengo la kuwainua wananchi wake kiuchumi ili waweze kuondokana na umaskini.


No comments: