Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
WANANCHI wanaoishi katika mikoa inayopakana na nchi ya Malawi
wamehimizwa kuona umuhimu wa kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini humo,
ikiwemo kufanya biashara kwa njia ambazo ni halali ili waweze kuinua uchumi
wao.
Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Hassan Bendeyeko alisema hayo
juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo
alisisitiza kuwa wananchi wanaoishi katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na
Ruvuma wanayo fursa kubwa ya kuweza kufanya hivyo ili waweze kuondokana na
umaskini.
Bendeyeko alisema kuwa hivi sasa ni wakati pekee wa
kuchangamkia fursa hizo kwa kujenga ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na
Malawi, jambo ambalo litaweza kuleta tija katika shughuli zao za kukuza uchumi wa
kila siku.
Alisema kuwa hivi karibuni alihudhuria mkutano wa ushirikiano
kati ya nchi ya Tanzania na Malawi ambao ulifanyika Jijini Lilongwe pamoja na
mambo mengine waliyozungumza kwenye mkutano huo, walizungumzia pia uwepo
wa fursa nyingi za kilimo, uvuvi, mifugo pamoja na biashara ambazo Watanzania
kwa kufuata taratibu husika wanaweza wakafanya shughuli za
kibiashara kwa kushirikiana na wananchi wa Malawi.
Pia alifafanua kwamba upande wa nchi hiyo ya Malawi kando kando
mwa ziwa Nyasa wamekuwa wakitumia fursa za kilimo, ufugaji pamoja na uvuvi
ambazo Watanzania waishio mikoa ya Songwe, Mbeya, Njombe na Ruvuma wakifanya
hivyo wataweza kukuza uchumi wao.
Katibu tawala huyo alieleza pia wananchi wa Malawi wameonesha
nia ya kutumia bandari ya Mtwara kwa kusafirisha bidhaa zao ambazo zitapitishwa
kwenye barabara ya kutoka Mtwara hadi Malawi, kupitia bandari ya Mbamba bay hivyo
wananchi wa maeneo hayo wanapaswa kuona umuhimu wa kutumia fursa hizo kwa
manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Vilevile aliongeza kuwa akiwa nchini Malawi walifanikiwa
kwenda Mzuzu kwenye gereza kuu ambako walikutana na Watanzania nane ambao
walitoka Songea mkoani Ruvuma kwenda Malawi, kufanya utafiti wa madini ya
Uranium ambapo walikamatwa wakidaiwa kuwa ni majasusi.
No comments:
Post a Comment