Tuesday, February 7, 2017

MADIWANI MBINGA WATAKIWA KUSIMAMIA KIKAMILIFU MIRADI YA WANANCHI

Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amewataka Madiwani wa wilaya hiyo kusimamia kikamilifu miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi ambayo inatekelezwa katika kata zao, ili iweze kukamilika kwa wakati na viwango vinavyokubalika.

Pia amewaasa wazingatie masuala ya kitaalamu pindi watendaji wanapotoa ushauri wakati huo wa utekelezaji wa miradi jambo ambalo litasaidia kuepusha migongano baina yao.

Nshenye aliyasema hayo juzi wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya kujenga uelewa kwa Madiwani wa halmashauri ya mji wa Mbinga juu ya sheria, kanuni na miongozo katika usimamizi na uendeshaji wa halmashauri yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.


Alisema kuwa serikali imekuwa ikitekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo jukumu la Madiwani ni kuhakikisha kwamba wanasimamia kikamilifu kazi zinazofanyika kwenye maeneo yao na kwamba pindi wanapoona kuna ubabaishaji katika utekelezaji huo wasisite kutoa taarifa kwenye vyombo husika ili viweze kuchukua hatua.

“Ninyi mmepewa dhamana kubwa na wananchi kwenye kata zenu mnapaswa kuhakikisha mnazingatia maadili ya kazi zenu za kila siku, lakini pia hamasisheni kupitia mikutano yenu ya wananchi ili waweze kubuni miradi yenye tija kwao na muisimamie kwa umakini ili kujenga imani kwa wananchi”, alisema Nshenye.

Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza juu ya umuhimu pia wa Madiwani hao kuhakikisha kwamba asilimia kumi inayotengwa kupitia mapato yao ya ndani kwa ajili ya wanawake na vijana, yanawafikia walengwa kama inavyosisitizwa siku zote na kwamba wawakumbushe kurejesha mkopo kwa wakati ili wengine nao waweze kunufaika nayo.

Nshenye alisema mahusiano mazuri baina ya Madiwani na watendaji yanapaswa kuimarishwa kwani kama patakuwa na mgongano baina yao watachangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inapaswa kwenda kwa wananchi.


Awali Katibu msaidizi maadili ya viongozi kutoka ofisi ya kanda Mtwara, Mayina Henjewele alizitaja mada zinazofundishwa kwenye mafunzo hayo kuwa ni maadili ya viongozi wa umma, mahusiano ya kazi kati ya madiwani na watumishi, maadili ya madiwani, sheria zinazosimamia serikali za mitaa, kanuni za kudumu za halmashauri, wajibu na majukumu ya madiwani na mipaka ya utendaji kazi wa madiwani.

No comments: