Na Kassian Nyandindi,
Songea.
SERIKALI kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Songea
mkoani Ruvuma, imetoa ufafanuzi juu ya hatua iliyochukua ya kuwafungia vibanda
Wafanyabiashara wa Soko kuu Songea lililopo katika Manispaa hiyo kwamba,
walifanya hivyo kutokana na wafanyabiashara hao kudaiwa shilingi milioni 150 za
pango la vibanda vya biashara ambavyo wamepanga.
Ufafanuzi huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Songea,
Pololet Kamando Mgema alipokuwa akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini
kwake katika ukumbi wa mikutano wa wilaya hiyo.
Mgema alifafanua kuwa soko hilo lilianzishwa mwaka 1938
na kwamba ulipofika mwaka 1996 halmashauri hiyo ililazimika kuwaruhusu
wafanyabiashara kukarabati vibanda hivyo vya soko ambavyo walikuwa wakifanyia
biashara zao.
Alisema kuwa kila mfanyabiashara kwa wakati huo alikuwa
akilipa pango la shilingi 8,000 kwa mwezi ambapo kiasi hicho kilikuwa
kikiendelea kulipwa mpaka Agosti 20 mwaka 2002 wakati soko hilo lilipoungua na
kuteketea kwa moto.
Mkuu huyo wa wilaya alibainisha kuwa baada ya kuungua
moto soko hilo halmashauri ya Manispaa ilifanyajitihada mbalimbali ya
kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kupata huduma kwenye soko hilo, ambapo
uongozi wa Manispaa ya Songea kwa kushirikiana na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la
Songea, Hayati Dkt. Laurence Gama waliomba fedha toka kwa wadau mbalimbali wa
maendeleo na kuweza kufanikiwa kujenga soko kuu la Songea.
Alisema waliochangia katika ujenzi huo ni Wizara ya
fedha kupitia shirika la Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) ambalo lilitoa shilingi milioni
304,228,270 Mkopo kutoka bodi ya mikopo serikali za mitaa ilitoa shilingi milioni
125,000,000 Mchango wa halmashauri ya Manispaa shilingi milioni 50,000,000 Japan
Food Aid shilingi milioni 133,944,060 na kuweza kufikia jumla ya shilingi milioni
613,172,330 ambazo zilifanya kazi ya ujenzi wa soko hilo.
Mgema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na
usalama ya wilaya ya Songea alisema kuwa baada ya kupata fedha hizo ujenzi wa
soko ulitekelezwa mara moja na kukamilika ambapo lilianza kutumika mwezi Mei mwaka
2004 na kwamba halmashauri hiyo kwa ujumla ilihusika na ujenzi huo kwa asilimia
mia moja na kuweza kuingia mkataba wa kuwapangisha wafanyabiashara hao.
“Manispaa ilijiwekea utaratibu wa kupandisha pango kila
baada ya miaka mitatu kulingana na kuongezeka kwa gharama
za uendeshaji, mkataba wa mwisho kati ya Manispaa na wafanyabiashara hawa
uliishia Juni 30 mwaka 2016 na kwamba kufikia mwezi Machi mwaka 2016 kabla ya mkataba
kwisha muda wake kiliundwa kikosi kazi cha kupitia na kuhakiki wapangaji wote
ili tuweze kujiridhisha ni nani anayetumia kibanda husika kutokana na kuwepo
kwa taarifa kwamba baadhi ya wapangaji, wamewamilikisha wapangaji wengine kwa
bei kubwa kuliko ile wanayolipa halmashauri na kusababisha kuwepo kwa msuguano
mkubwa kati yao na uongozi wa Manispaa”, alisema Mgema.
Alieleza kuwa hadidu rejea zilizotumika na kikosi kazi hicho
ziliweza kuwatambua wapangaji halali wa vibanda vyote 270 na kuainisha bei
halisi ya sasa iliyopangwa na Manispaa na bei wanayopangishwa wapangaji halali
kwa wapangaji wengine.
Pia aliongeza kuwa kufuatia kuwepo kwa hali hiyo wiki
moja iliyopita serikali kwa kushirikiana na halmashauri hiyo baada ya kuona
hivyo ililazimika kuvifunga vibanda vyote mpaka wafanyabiashara hao, walipe
deni hilo wanalodaiwa ili halmashauri iweze kupunguza deni la mkopo iliochukua
wakati wa kujenga soko hilo kutokana na kuteketea kwa moto.
Chiunga alisema halmashauri imepangisha pango kwa
asilimia mia moja, wakati vibanda hivyo baada ya kuungua soko
vilijengwa na wafanyabiashara wenyewe kwa makubaliano kwamba vikikamilika ujenzi
wake nusu ya pango itakuwa inatolewa kwenda halmashauri na nusu nyingine
inafidia ujenzi husika wa vibanda, hivyo ameiomba serikali iangalie namna ya
kukaa pamoja na suluhisho sio kuendelea kuvifunga kwani wafanyabiashara wanaendelea
kupata hasara.
No comments:
Post a Comment