Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linawashikilia wakazi wawili wanaoishi
katika mtaa wa Pambazuko uliopo katika kata ya shule ya Tanga Manispaa ya
Songea mkoani humo, kwa tuhuma ya kumjeruhi Abethi Ponera (25) kwa kumkata na
kitu chenye ncha kali kwenye paja lake la mguu upande wa kulia na kumsababishia
jeraha na maumivu makali.
Zubery Mwombeji. |
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji amewataja
watuhumiwa hao kuwa ni Bernad Mng`ong`o (39) na Boniface Mbecha (27) wote
wakazi wa mtaa huo.
Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 21 mwaka
huu majira ya saa tano usiku, katika mtaa huo.
Alifafanua kwamba siku ya tukio hilo Ponera akiwa anarudi
nyumbani kwake akitokea kunywa pombe kwenye kilabu cha pombe za kienyeji, ghafla
alivamiwa na watu asiowafahamu na kuanza kumpiga kisha kumjeruhi paja lake la
mguu wa kulia na kuathiri sehemu zake za siri.
Alisema kuwa Ponera kabla ya kukutwa na tukio hilo akiwa
katika kilabu hicho ambacho kinamilikiwa na Mg’ong’o kulikuwa na malumbano kati
yake na watu wengine aliokuwa anakunywa nao pombe hizo za kienyeji, ambao
walikuwa wakimtaka ifikapo Januari 22 mwaka huu aende kwenye uchaguzi mdogo
akamchague mgombea udiwani wanayemtaka wao (chama ambacho jina lake
linahifadhiwa) jambo ambalo Ponera alipingana nalo kisha baadaye aliamua
kuondoka kuelekea nyumbani.
Alieleza zaidi kuwa askari Polisi waliokuwa doria siku hiyo walimkuta
Ponera akiwa njiani amelala huku damu zikimtoka kutokana na jeraha kubwa alilokuwa
nalo.
Vilevile aliongeza kuwa askari hao walimchukua na kwenda naye
hadi kituo kikuu cha Polisi ambako alipatiwa hati ya matibabu na baadaye
alipelekwa hospitali ya Rufaa Songea ambako amelazwa akiendelea kupatiwa
matibabu.
Pia Kamanda Mwombeji alieleza kuwa uchunguzi wa awali
umebaini kwamba kabla ya Ponera kujeruhiwa kutokana na kuwa katika kilabu hicho
mmiliki wa kilabu hicho, Mg’ong’o na mwenzake Mbecha waliwakamata kwa mahojiano
zaidi na upelelezi utakapokamilika watafikishwa Mahakamani.
No comments:
Post a Comment