Na Kassian Nyandindi,
Songea.
POLOLET Kamando Mgema, ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Songea
mkoani Ruvuma amewapongeza walimu wa shule za msingi na sekondari katika
Manispaa ya Songea mkoani humo, kwa kufanya kazi nzuri ambayo imeleta mafanikio
mazuri ya kukuza taaluma katika matokeo ya mitihani darasa la saba na kidato
cha nne.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa pongezi hizo kwenye kikao cha
tathimini ya elimu kwa mwaka wa 2015/2016 ambacho kiliwakutanisha Wadau mbalimbali
wa elimu Waratibu elimu kata, Walimu wakuu wa shule za msingi, Wakuu wa shule
za sekondari, Madiwani na Maofisa elimu ambacho kilifanyika kwenye ukumbi wa
shule ya sekondari ya wasichana Songea.
Pamoja na kuwapatia pongezi hizo, Mgema alikemea pia tabia
zinazofanywa na baadhi ya walimu kuwa na utoro kazini ambapo amewataka waache
mara moja vinginevyo kwa yule atakayebainika hatua kali za kisheria
zitachukuliwa ikiwemo kufukuzwa kazi.
Kwa upande wake Ofisa elimu sekondari Manispaa ya Songea
Devotha Luongo alisema kuwa hatakubaliana na vitendo vitakavyofanywa na mwalimu
yeyote ambaye ataonesha udhaifu kwenye maeneo yake ya kazi kwa mambo ya ulevi
na utoro kazini vinginevyo ajiondoe mwenyewe mapema.
Luongo alisema kuwa amefurahishwa na matokeo ya mitihani ya
kidato cha nne katika kipindi cha mwaka jana ambapo wanafunzi walioshika nafasi
za kwanza kimkoa kwenye mtihani wa Fizikia na Mtihani wa Kemia walitoka shule
za sekondari za Manispaa ya Songea, hivyo ni vyema Wadau wa elimu wakiwemo
wazazi wanapaswa kuendelea kuwahimiza watoto wao kusoma kwa bidii na sio
kuwaacha mitaani wakizurula.
Editha Kagomba ambaye naye ni Ofisa elimu kwa shule za msingi
katika Manispaa hiyo alisema kuwa asilimia 55 ya wanafunzi wa shule hizo
wamekuwa wakihudhuria masomo darasani lakini kumekuwa na wale ambao ni watoro hawahudhurii
masomo hayo ambapo wamefikia asilimia 45.
Aliwataka Walimu wakuu kwa shule za msingi pamoja na Waratibu
elimu kata kuona umuhimu wa kuhimiza wazazi kujenga mahusiano mazuri kati yao
na walimu kwa lengo la kuhakikisha watoto wote wanakwenda shule na kwamba
ameiomba serikali kuendelea kuajiri walimu katika shule hizo ili kuweza
kupunguza tatizo la uhaba wa walimu lililopo sasa.
No comments:
Post a Comment