Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Omary Likande (32)
ambaye ni mkazi wa kijiji cha Msechela wilayani Tunduru mkoani humo, kwa tuhuma
ya kumuua mdogo wake Unda Likande (23) kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali
shingoni.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kamanda wa Polisi wa
mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 7 mwaka
huu majira ya mchana katika kitongoji cha Mkalala kilichopo katika kijiji cha Msechela
tarafa ya Namasakata wilayani humo.
Mwombeji alisema kuwa siku hiyo ya tukio inadaiwa kuwa Unda
aliuawa kwa kukatwa shingoni na kaka yake, Omary Likande wakati baba yao alipokuwa
ametoka kwenda kutafuta chakula.
Alifafanua kuwa tukio hilo lilitokea kwenye kibanda ambacho
kipo katikati ya shamba la wazazi wao ambapo Omary baada ya kumuua mdogo wake
aliendelea kubaki kwenye eneo hilo mpaka baba yao alipofika na kuona mtoto wake
mmoja akitokwa na damu nyingi shingoni.
Alisema kuwa baadaye baba yao alipoona hivyo alitoa taarifa
kwa uongozi wa serikali ya kijiji ambao nao ulitoa taarifa kwenye Kituo kikuu cha
Polisi wilayani Tunduru na askari walipowasili kwenye eneo la tukio wakiwa
wameongozana na daktari ambaye alithibitisha kuwa Unda Likande amefariki dunia
kwa kuchomwa na kitu hicho chenye ncha kali.
Jeshi hilo la Polisi limesema kuwa uchunguzi wa awali
umebaini kuwa mtuhumiwa Omary Likande ana tatizo la muda mrefu la ugonjwa wa
akili ambao huenda ukawa ndiyo chanzo cha tukio hilo.
No comments:
Post a Comment