Sehemu ya watumishi wa halmashauri ya wilaya Mbinga, wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo Cosmas Nshenye. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye
amesema kuwa katika wilaya hiyo kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa
wananchi ambayo amekuwa akiyapokea kwa nyakati tofauti kwamba katika vituo vya
kutolea huduma za afya wilayani humo, kumekuwa na tatizo la ukosefu wa dawa
jambo ambalo limekuwa ni kero kubwa kwa wananchi.
Aidha kufuatia hali hiyo amewataka watendaji waliopewa
dhamana kusimamia kikamilifu majukumu yao ya kazi ikiwemo kujipanga ipasavyo
katika kuhudumia wagonjwa wanaokwenda kutibiwa ili kuweza kuondoa malalamiko
hayo yasiyokuwa ya lazima.
Nshenye alisema kuwa tatizo hilo linaanzia hospitali ya
wilaya ambapo malalamiko juu ya ukosefu wa dawa yamekuwa yakitolewa na wananchi
kwa muda mrefu na kwamba wamekuwa wakilazimika wakati mwingine kwenda kununua
dawa hizo kwenye maduka ya dawa muhimu badala ya kupewa hospitalini hapo.
Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, Nshenye alisema hayo juzi wakati
alipokuwa akihutubia katika baraza la Madiwani wa halmashauri ya mji wa Mbinga
ambalo lilifanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.
Pia alisema kuwa anachukizwa na tabia kwa baadhi ya Waganga
wafawaidhi kutokuwepo masaa ya kazi katika vituo vyao vya kutolea huduma za
afya, hivyo amekemea tabia hiyo na kuwataka waache mara moja na badala yake
wakae katika vituo hivyo ili waweze kuhudumia wagonjwa.
Hata hivyo aliongeza kuwa hali hii inaonesha kwamba watendaji
hao wa serikali hawajajipanga vizuri katika kuhudumia wananchi na kwamba ofisi
yake iwe ni mwisho kusikia au kuona maeneo ya kutolea huduma za afya kwamba
hayana dawa.
No comments:
Post a Comment