Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amewapongeza
wajumbe wa kikao cha maridhiano ya kugawana mali kati ya pande mbili za
halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga kwa kumaliza kikao hicho
katika hali ya amani, utulivu na maelewano bila ya kuwepo kwa mgogoro, mvutano
na malumbano.
Cosmas Nshenye. |
Nshenye ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, alitoa
pongezi hizo juzi wakati alipokuwa akizungumza na Madiwani wa halmashauri hizo
katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.
Alisema kuwa kitendo hicho kimeonyesha utashi na ukomavu wa
kifikra kwa kile alichoeleza kuwa kuna baadhi ya maeneo mengine wanapokuwa
kwenye vikao kama hivyo, imekuwa ikizuka migogoro na malumbano ambayo
yanachangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi huku
akisisitiza kuwa uhamisho wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga utafanyika mara
baada ya kukamilika kwa ujenzi wa ofisi zao.
Akichangia hoja kwenye kikao hicho, Mwenyekiti wa halmashauri
ya mji wa Mbinga Kipwele Ndunguru alisema kuwa mapendekezo yaliyoridhiwa na
kikao cha kamati ya ushauri ni kuhamisha bajeti ya shilingi bilioni 2.1 ambayo
ilikuwa inatakiwa kujenga boma la halmashauri hiyo na kuzihamishia halmashauri
ya wilaya ya Mbinga ambapo mpaka sasa kwa kuanzia kimetolewa kiasi cha shilingi
milioni 500.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Ambrose
Nchimbi alisema kuwa kwa upande wa baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo pia wameridhia
kutoa mali zote zisizohamishika na kuzikabidhi kwa halmashauri ya mji wa
Mbinga.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mbinga mjini, Sixtus
Mapunda alipongeza jitihada zilizofanyika kwa kumaliza suala hilo kwa maelewano
mazuri katika kushughulikia suala la mgawanyo wa mali jambo ambalo alidai kuwa
awali lilikuwa linakwamisha kufanya shughuli za maendeleo huku Mkurugenzi wake mtendaji
wa halmashauri hiyo, Robert Mageni akiwaomba Madiwani wa halmashauri ya mji huo
kuendelea kujenga umoja na mshikamano.
No comments:
Post a Comment