Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA kuhakikisha kwamba wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma, wanaendelea kunufaika na uzalishaji wa zao la kahawa wilayani humo,
wilaya inaendelea kutekeleza mpango wa kuhifadhi na kuuza kahawa ikiwa na jina
la Ex Mbinga, badala ya Miji ya Makambako mkoani Njombe kama ilivyokuwa hapo
awali.
Aidha mpango huo wa kuuza kahawa kwa majina ya Ex Makambako
ulikuwa ukisababisha kupunguza faida ya mauzo ya kahawa kwa mkulima na
kuhamasisha wafanyabiashara kutorosha kahawa ya Mbinga na kumfanya mkulima
aendelee kupata hasara.
Taarifa hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas
Nshenye ambapo alifafanua kuwa gharama hizo kwa mkulima hivi sasa zimepungua
ikiwemo na suala la utoroshaji wa kahawa, hali ambayo inavutia hata kuwepo kwa
wawekezaji wa zao hilo wilayani humo.
Vilevile akizungumzia juu ya mwenendo wa uzalishaji wa mazao
ya chakula na biashara, Nshenye alisema kuwa kiwango cha uzalishaji wa mazao
hayo kimeongezeka kutokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa na kutekelezwa
ikiwemo kuongezeka kwa matumizi ya mbegu bora, uhamasishaji wa kilimo cha
kahawa, korosho na zao la mpunga uliofanywa na wilaya kwa kushirikiana na wadau
wa kilimo.
Nshenye aliongeza kuwa kutolewa kwa elimu ya ugani kwa
wakulima na uwepo wa pembejeo za ruzuku nao umechangia kwa kiasi kikubwa
uzalishaji huo kuwa wenye tija katika jamii.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa wilaya ya Mbinga ina jumla
ya vyama vya ushirika 63 vyenye wanachama 13,716 ambapo vya akiba na mikopo
yaani SACCOS navyo vipo 34 vyenye wanachama 33,757 wenye jumla ya hisa shilingi
milioni 184,598,800.
Kadhalika alieleza kuwa mikopo iliyotolewa mpaka sasa katika
vyama hivyo ina jumla ya shilingi bilioni 8,220,702,457 na kwamba sehemu ya
mikopo iliyorejeshwa ni shilingi bilioni 4,394,414,162 hivyo bado kurejeshwa
mikopo ya shilingi bilioni 3,826,288,295.
No comments:
Post a Comment