Tuesday, February 14, 2017

WALIOCHUKUA MIKATABA SOKO KUU SONGEA WAANZA KUFUNGULIWA VIBANDA VYAO

Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,  Abdul Hassan Mshaweji amesema kwamba tayari vibanda vya Soko kuu la Manispaa hiyo vimeanza kufunguliwa na kupewa wafanyabiashara ambao wametimiza masharti yaliyowekwa na Manispaa hiyo.

Pololet Mgema, Mkuu wa wilaya ya Songea.
Kufunguliwa kwa vibanda hivyo alieleza kuwa kunafuatia wafanyabiashara wa Soko hilo ambao baadhi yao wamekubali kuingia mkataba mpya na halmashauri hiyo na kulipia gharama ya pango katika kibanda husika.

Mshaweji alifafanua kuwa hadi mwishoni mwa wiki hii wanatarajia idadi kubwa ya vibanda vitakuwa vimefunguliwa, baada ya wafanyabiashara wengi kuhamasika kuchukua mikataba na kulipia kodi ya vyumba vilivyopo katika soko hilo. 

Alisisitiza kuwa Manispaa inatekeleza kwa vitendo maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kuhakikisha kwamba Soko kuu la Manispaa ya Songea linakuwa chanzo muhimu cha mapato kwa lengo la kukuza uchumi wa Manispaa hiyo.


Kadhalika akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema alisema kuwa serikali inafanya hivyo kwa lengo la kutekeleza kwa vitendo, maagizo hayo ya Waziri mkuu ambayo aliyatoa hivi karibuni wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa.

Mgema alisema kuwa Majaliwa aliagiza kuwatambua wakodishaji wote wa vibanda vya Soko hilo na kuweka mkataba kati ya halmashauri ya Manispaa ya Songea na anayetumia kibanda husika.

Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza kwamba katika upangishaji wa vibanda hivyo asiruhusiwe mtu wa kati (Middle man) wakati upangishaji huo unapofanyika.

Alisema kuwa kinachofanyika hivi sasa ni utekelezaji wa maagizo hayo na kwamba serikali inasimamia kwa nguvu zote baada ya kujiridhisha kwamba Soko hilo limejengwa na Manispaa kwa asilimia 100 na kwamba, kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wajanja wakinufaika kwa kumpangisha mtu wa kati kwa gharama kubwa.

Pamoja na mambo mengine, awali Wafanyabiashara wa halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani humo juzi walituma ujumbe wa wafanyabiashara wenzao watano na wazee watano kwenda Dodoma kumuona Waziri Mkuu, Majaliwa kwa lengo la kupeleka kilio chao baada ya Mkuu wa wilaya ya Songea Mgema kuwafungia vibanda hivyo vya biashara, tangu Februari 11 mwaka huu kwa madai kwamba wanadaiwa shilingi milioni 100 na halmashauri hiyo jambo ambalo walikana na kueleza kuwa sio la kweli.

Vilevile Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Masoko katika Manispaa hiyo (UWABIMASO) Leonard Chiunga alisema kuwa maduka 275 ambayo yapo kwenye vibanda vya soko hilo mjini hapa, yalifungwa na Mkuu huyo wa wilaya ya Songea akiwa ameongozana na Kamati yake ya ulinzi na usalama kwa madai kwamba wafanyabiashara hao wanatakiwa waingie mikataba upya na halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa lazima na pango la vibanda hivyo inabidi lipande kwa asilimia mia moja jambo ambalo alisema kuwa ni kinyume na makubaliano ya vikao mbalimbali vilivyofanyika hapo awali.

No comments: