Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa katika mkoa wa Ruvuma wilaya ya Mbinga mkoani
humo imekuwa ikiongoza kwa kilimo cha bangi, hivyo serikali itaendelea
kupambana na watu wanaohusika na uzalishaji wa zao hilo kwa kuwachukulia hatua
za kisheria ikiwemo kuwafikisha Mahakamani.
Aidha wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano mara kwa mara kwa
viongozi wa ngazi ya vijiji, kata hadi wilaya katika utoaji wa taarifa ni wapi
kumekuwa na mashamba ambayo yamekuwa yakitumika kuzalisha zao hilo.
Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alisema hayo jana
alipokuwa akizungumza na Madiwani pamoja na wananchi kwenye kikao cha kujadili
mapendekezo ya mpango wa bajeti ya maendeleo halmashauri ya mji wa Mbinga kwa
mwaka wa fedha wa 2017/2018 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo
mjini hapa.
“Vita ya madawa ya kulevya ni kubwa hata hapa kwetu ipo,
tatizo hili tayari wengine tumewafikisha Mahakamani na wengine bado
tunawachunguza natoa wito kwenu sisi sote ni wadau katika kupambana nalo”, alisisitiza
Nshenye.
Nshenye alifafanua kuwa anatambua kwamba Madiwani, Watendaji
wa vijiji na kata katika maeneo yao wamekuwa wakifahamu watu wanaohusika na
usambazaji wa madawa hayo ya kulevya, hivyo wanapaswa kutoa taarifa hizi kwenye
vyombo vya dola ili hatua ziweze kuchukuliwa mapema.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho
kufanyika naye diwani wa kata ya Mpepai, Benedict Ngwenya alieleza kuwa bangi
katika wilaya ya Mbinga imekuwa ikizalishwa hasa katika kata yake kutokana na
kata hiyo kuwa na mapori makubwa ambayo yamepakana na hifadhi ya wanyama ya
Liparamba.
Ngwenya aliongeza kuwa pia katika hifadhi hiyo baadhi ya watu
ambao ndio wanaendekeza kilimo cha zao hilo wamekuwa wakiingia ndani ya msitu
wa hifadhi na kulima bangi na kwamba ameiomba serikali ifanye oparesheni
maalumu ya kuchunguza kwa kina na kuwabaini ili hatimaye kuteketeza kabisa
kilimo hicho kisiweze kuendelea na kuathiri jamii hasa vijana ambao ndiyo
tegemeo la kukuza uchumi kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
No comments:
Post a Comment