Na Mwandishi wetu,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Suzana Mgaya (19)
ambaye ni mkazi wa kijiji cha Wino tarafa ya Madaba wilayani Songea mkoa wa
Ruvuma, kwa tuhuma ya kumnywesha sumu mwanaye mwenye umri wa mwaka mmoja na
nusu aliyejulikana kwa jina la Gerlad Kabelege na kusababisha afariki dunia huku
yeye mwenyewe pia akinywa sumu hiyo kwa lengo la kutaka kujiua.
Taarifa zilizopatikana jana mjini Songea na kuthibitishwa na Kamanda
wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Februari
5 mwaka huu majira ya saa 12:00 jioni katika kijiji hicho cha Wino.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa
Suzana Mgaya siku hiyo alikutwa akitoka povu mdomoni na puani jambo ambalo
lilisababisha hofu kwa mashuhuda kuwa huenda amekunywa sumu.
Mwombeji alifafanua mashuhuda hao walimkuta Mgaya akiwa
mahututi baada ya kuvunja mlango wa nyumba yake ambao alikuwa ameufunga kwa
ndani na kwamba juhudi za kuwaokoa zilifanyika kwa kuwatoa ndani ya nyumba hiyo
kisha kuwapeleka kwenye zahanati ya kijiji cha Wino ambapo mtoto Gerlad alifariki
wakati akipatiwa matibabu.
Akifafanua juu ya tukio hilo Kamanda Mwombeji alisema kuwa
Mgaya baada ya kuonekana hali yake inaendelea kuwa mbaya alikimbizwa kwenye
kituo cha afya cha Madaba ambako alipatiwa rufaa ya kwenda hospitali ya
serikali ya mkoa huo iliyopo mjini hapa na kufikishwa kwenye chumba cha
wagonjwa mahututi na baadae aliweza kupata nafuu.
Alisema mpaka sasa Jeshi la Polisi linaendelea kumshikilia
mtuhumiwa huyo akiwa hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kwamba
mara baada ya uchunguzi huo kukamilika atafikishwa Mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
Kadhalika uchunguzi wa mwili wa mtoto huyo baada ya kufariki
dunia ulifanyika katika kituo cha afya cha Madaba na kuweza kubaini kuwa kitu alichokuwa
amemnyeshwa inadaiwa kuwa ni sumu ambapo taarifa zitatolewa baadaye kuwa
ilikuwa ni ya aina gani.
No comments:
Post a Comment