Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.
WAJUMBE Kamati ya
uongozi na mipango katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
imepongeza kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Kampuni ya Sinani Building
Contactors katika kukamilisha ujenzi wa nyumba za walimu shule ya sekondari
Kitura iliyopo wilayani humo, mradi ambao hadi kukamilika kwake utagharimu
shilingi milioni 168.7.
Mwenyekiti wa
kamati hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Ambrose
Nchimbi alitoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kukagua mradi huo iliyofanyika
mwishoni mwa wiki ambapo alisema kwamba mradi huo hadi kukamilika kwake utasaidia
kuondoa tatizo la walimu kukosa nyumba za kuishi na kuondokana na adha ya kupanga
uraiani.
Nchimbi alisema
kuwa mradi huo unagharimu fedha nyingi hivyo ni vyema ujenzi wake unapaswa kuwa
wa viwango vinavyokubalika na kwamba kamwe halmashauri hiyo, haitawavumiliwa makandarasi
ambao wamekuwa na tabia ya kuhujumu miradi ya maendeleo ya wananchi na
kusababisha kuzua malalamiko yasiyokuwa ya lazima.
“Nimekuja hapa
kukagua ujenzi wa nyumba hizi za walimu kimsingi tumeridhishwa na viwango vya
ujenzi wa jingo hili sasa niwaombe kamilisheni kwa wakati, ili hatimaye walimu
waweze kuhamia hapa na kuanza kuishi katika nyumba hizi”, alisema Nchimbi.
Naye mjumbe wa
kamati hiyo, Zena Mijinga pamoja na kupongeza kazi nzuri inayoendelea kufanyika
katika utekelezaji wa mradi huo alishauri kwamba viongozi wa kata hiyo akiwemo diwani
na mtendaji wanapaswa wahakikishe wanatembelea eneo hilo mara kwa mara ili
kujiridhisha na kazi hiyo ya ujenzi unaoendelea kufanyika hapo ili iweze kwenda
sambamba na malengo husika.
Zena alisema kuwa
serikali itaendelea kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi mara
kwa mara kwa lengo la kujionea na kujiridhisha kama kweli inatekelezwa kwa
viwango vinavyokubalika huku akiitaka kampuni hiyo ya Sinani ihakikishe inaendelea
kufanya kazi hiyo kwa uaminifu na maelekezo iliyopewa.
No comments:
Post a Comment