Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amewajia
juu watendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo ambao wanadaiwa kuhusika kwa namna
moja au nyingine kufanya ubadhirifu wa fedha shilingi bilioni 1.4 ambazo
zilitolewa na serikali kwenda wilayani humo, kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
kwa ajili ya kufanya kazi iliyolengwa katika uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba
25 mwaka jana.
Ngaga alisema kuwa ubadhirifu huo umebainika, baada ya ofisi
yake kuunda tume ndogo ambayo ilifanya kazi kwa ushirikiano wa baraza la kamati
ya ulinzi na usalama la wilaya hiyo na kuweza kubaini wizi huo, uliofanyika
katika fedha hizo za serikali.
Senyi Ngaga, Mkuu wa wilaya ya Mbinga. |
Aidha alisema kuwa tume hiyo iliyoundwa ambayo inaendelea na
uchunguzi wake na majina ya waliohusika kuwekwa bayana hapo itakapomaliza kazi
yake, ambapo taarifa za awali katika fedha hizo zinathibitisha kwamba maofisa
waliopewa dhamana ya kuendesha uchaguzi huo wilayani hapa kwa kushirikiana na
idara ya fedha na manunuzi ya wilaya hiyo, ndio wanaodaiwa kuhusika kutengeneza
mianya ya kutafuna fedha hizo.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Ngaga kwenye kikao cha
baraza la Madiwani wilayani humo kilichoketi juzi kwenye ukumbi wa Umati uliopo
mjini hapa na kwamba alieleza kuwa ubadhirifu huo umefanyika kupitia watu
kulipana posho, ununuaji wa mafuta na vipuri vya magari, chakula na vifaa vingine
vya ofisi (Stationary) kinyume na taratibu za miongozo iliyotolewa na serikali.
Mkuu huyo wa wilaya alifafanua kuwa mpaka sasa kati ya fedha
hizo zilizotolewa na NEC wameweza kubaini ubadhirifu wa shilingi milioni 513
ambazo hazikufuata taratibu na miongozo husika katika matumizi yake, ambapo
kati ya hizo shilingi milioni 822 zimetumika watu kulipana posho, shilingi milioni
140 kwa ajili ya kusambaza vifaa vya maofisini, shilingi 135 zimetumika kununua
vipuri vya magari na mafuta na kwamba shilingi milioni 85 zimetumika kwa ajili
ya chakula.
Akielezea juu ya fedha zilizotumika kununulia vifaa vya ofisi
shilingi milioni 140, alisema kuwa tume hiyo aliyoiunda kuchunguza matumizi ya
fedha hizo imebaini kuwa fedha zilizotumika kununulia vifaa hivyo ni shilingi
milioni 4 tu na sio zaidi ya fedha hizo, ambapo suala hilo lilithibitishwa
baada ya tume kumhoji mzabuni husika ambaye alipewa kazi ya kusambaza vifaa
hivyo vya ofisini.
Vilevile alieleza kuwa fedha zilizotumika kununulia vipuri
vya magari shilingi milioni 135 mzabuni aliyetumika kufanya kazi hiyo, hana
duka au kampuni ambayo ingeweza kumfanya aweze kuwa na sifa katika mchakato wa
manunuzi ya vifaa husika jambo ambalo linaleta mashaka na kujenga mianya ya
wizi wa fedha za umma.
“Mheshimiwa Mwenyekiti hali hii inasikitisha sana, hata
mafuta yaliyonunuliwa kwa ajili ya kufanikisha zoezi la uchaguzi mkuu cha
kushangaza katika taarifa za fedha baada ya tume yangu kuchunguza, imegundua
kwamba mafuta mengine yalitumika kujaza kwenye katapila la halmashauri, malori
ya kubeba mizigo na pikipiki wakati huo wahusika waliopewa dhamana ya kusimamia
jambo hili wakijua kwamba hayahusiki kwenye shughuli za uchaguzi”, alisema
Ngaga.
Ngaga aliongeza kuwa ameshangazwa na ofisi ya Mkaguzi wa
ndani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, kutofanyia kazi jambo hilo na kutolea
taarifa katika vikao vya baraza la madiwani huku akiagiza na kumtaka mkaguzi
huyo wa ndani wilayani humo, kuhakikisha kwamba kuanzia sasa anafanya kazi zake
kwa uwazi na sio kuficha ukweli wa ubadhirifu wa fedha ambao hufanywa na
watumishi wasio kuwa waaminifu katika halmashauri hiyo.
“Kwa nini nimesema hivyo, ndugu zangu nimesema hivyo ili
madiwani muweze kuelewa vyombo vya dola vinaendelea na kazi yake hatutaishia
hapa jambo hili tutalifikisha mpaka ngazi ya juu na wale waliohusika kufanya
ubadhirifu huu watavuna walichopanda sipendi kumuonea mtu, watumishi wa
serikali fanyeni kazi kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa tuache kufanya kazi
kwa mazoea”, alisisitiza.
Kufuatia hali hiyo, kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri
ya wilaya ya Mbinga, Ambrose Mtarazaki alimuagiza kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo Samwel Komba kuhakikisha kwamba suala hilo anajenga
ushirikiano wa karibu na ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo, ili liweze kufanyiwa
kazi haraka na wahusika waliofanya ubadhirifu huo wachukuliwe hatua kwa mujibu
wa taratibu na sheria za nchi ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia
kama hiyo.
No comments:
Post a Comment