Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WAKULIMA wanaozalisha zao la kahawa wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma, wameshauriwa kuendelea kutumia miche bora ya kahawa aina ya vikonyo
ambayo haishambuliwi na wadudu waharibifu kwa urahisi na wakati wa mavuno,
huwafanya waweze kupata mazao mengi shambani.
Aidha Taasisi ya utafiti wa zao la kahawa (TaCRI) wilayani
humo, imepongezwa kwa jitihda zake inazoendelea kuzifanya, kwa kutoa elimu kwa
wakulima wa zao hilo hususan katika uzalishaji wa miche hiyo bora ya kahawa
ambayo huwaletea tija kubwa wakulima na kuwafanya waondokane na umaskini.
Hayo yalisemwa na mkulima mmoja maarufu wa zao hilo kutoka
kijiji cha Sepukila kata ya Kilimani wilayani hapa, Festo Mapunda alipokuwa
akihojiwa na waandishi wa habari juu ya uendelezaji wa kilimo bora cha zao hilo
katika wilaya ya Mbinga.
“Mimi binafsi naishukuru taasisi hii ya TaCRI, kwa kutupatia
elimu ya kilimo bora cha kahawa, hivi sasa wakulima tunaweza kuzalisha miche ya
vikonyo na kutoa ushauri juu ya kilimo bora cha zao hili kwa wengine ambao
wanapenda kulima kahawa”, alisema Mapunda.
Mapunda aliongeza kuwa yeye ana ekari nne za kahawa bora,
ambazo huzalisha zao hilo kwa wingi kila mwaka na kwamba kwa upande wa
uzalishaji wa miche ya vikonyo, ameanzisha shamba darasa ambalo linawanachama
42 wanaojishughulisha na uzalishaji wa zao hilo.
Alisema kuwa shamba darasa hilo linafahamika kwa jina la
Mitenga, limesajiliwa kisheria ambapo uzalishaji wa miche hiyo wamekuwa
wakiufanya kila mwaka kwa ajili ya kuwauzia wakulima wengine.
Pia alifafanua kuwa pamoja na kujikita katika uzalishaji wa
zao hilo, vilevile wamekuwa wakijishughulisha na kazi ya utunzaji wa mazingira
kwa kupanda miti rafiki ya maji, kwenye vyanzo vya maji na vilele vya milima.
Hata hivyo alibainisha kwamba hivi sasa wana shamba la miti
zaidi ya ekari 10 hivyo ametoa mwito kwa wananchi wengine kujitokeza kwa wingi
na kwenda kujifunza shughuli za kilimo bora cha kahawa na upandaji wa miti,
unaofanywa na kikundi hicho cha shamba darasa Mitenga kilichopo katika kijiji
cha Sepukila kata ya Kilimani wilayani Mbinga.
No comments:
Post a Comment