Na Kassian Nyandindi,
Njombe.
MAMLAKA ya Chakula, Dawa na Vipodozi (TFDA) Kanda ya nyanda
za juu Kusini imeteketeza kilo 1,000 za bidhaa aina mbalimbali, Halmashauri ya
wilaya na mji wa Njombe mkoani hapa, ambazo zimekwisha muda wa matumizi yake
kwa binadamu zenye thamani zaidi ya shilingi milioni 10.
Uteketezaji wa bidhaa hizo unafuatia msako mkali ulioendeshwa
na mamlaka hiyo kwa muda wa siku mbili, baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria
wema kwamba maduka mengi yaliyopo mkoani humo baadhi yake yamekuwa yakiuza
bidhaa zilizopitwa muda wa matumizi yake.
Kaimu Mkuu wa mkoa wa Njombe, Anatory Choya amewatahadharisha
wananchi wa mkoa huo kuwa makini na bidhaa hizo huku akikemea tabia ya
wafanyabiashara kuacha mara moja, kuuza bidhaa zilizopitwa na wakati kwani
wamekuwa wakihatarisha usalama wa afya za watumiaji.
Aidha Choya alisema kuwa msako huo utakuwa endelevu kwa
kupita kukagua kila duka lililopo mkoani humo, ikiwa pia ni lengo la kutokomeza
kabisa tabia kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa hizo zilizopigwa
marufuku na serikali.
Kaimu Mkuu huyo wa mkoa alisisitiza kwa kuwataka wataalamu wa
TFDA kuendelea na zoezi hilo na kwamba, pale wanapowakamata wafanyabiashara
wanaofanya hivyo wawafutie leseni zao za biashara ili iwe fundisho kwa wengine
wenye tabia kama hiyo ya kuendelea kuuza bidhaa hizo.
''Niwatahadharishe wananchi na wafanyabiashara wote wa mkoa
wa Njombe kitendo cha kuendelea kuuza bidhaa hizi feki ambazo zimepitwa na
wakati ni kuwaumiza watumiaji, wafanyabiashara mnatakiwa kuacha tabia ya kuuza
bidhaa zilizokwisha muda wake”, alisema Choya.
Choya alifafanua kwamba wafanyabiashara wengi wanaouza bidhaa
hizo wamekuwa wajanja, ambapo wao wenyewe wamekuwa hawazitumii badala yake
wamekuwa wakiwauzia wananchi kwa lengo tu la kutaka kupata faida jambo ambalo ni
hatari kwa watumiaji.
Pamoja na mambo mengine, aliongeza kuwa kuna kila sababu kwa
Mamlaka ya chakula, dawa na vipodozi hapa nchini kufungua ofisi zao katika kila
mkoa na kujiwekea utaratibu wa kupitia mara kwa mara maduka ya wafanyabiashara,
ili kuweza kudhibiti hali hiyo isiweze kuendelea kushamiri na kuumiza wananchi.
"Pale mnapobaini wafanyabiashara wanakiuka kanuni na
sheria toeni taarifa kwenye vyombo vya dola, ili serikali iweze kuchukua hatua
za kisheria kwa lengo la kuweza kudhibiti tabia hii ya wafanyabiashara
kuendelea kuuza bidhaa zilizopitwa na wakati”, alisisitiza.
Naye Meneja wa Mamlaka hiyo Kanda ya nyanda za juu kusini, Rodney
Alananga alisema kuwa wamefanikiwa
kukamata watu 57 katika Halmashauri ya
mji na wilaya ya Njombe katika maduka yao, wakiuza bidhaa feki zilizopitwa na
wakati.
Alisema kuwa katika msako huo walifanikiwa kukamata na
kuteketeza majani ya chai, pipi za aina mbalimbali, maziwa ya watoto, vipodozi,
vinywaji aina ya red bull na pombe kali aina ya viroba ambavyo vimetoka nchi
jirani ya Malawi.
Hata hivyo Alananga alisema kuwa bidhaa zilizopita muda wake
ni hatari kwa matumizi ya binadamu kwani zina sumu ambayo ni hatari kwa
mtumiaji, huku akisisitiza kwa kuwataka wananchi wanapokwenda kununua bidhaa
yoyote dukani kujenga mazoea ya kusoma mwisho wa tarehe ya matumizi, ili waweze
kuepukana na madhara yanayoweza kuwapata hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment