Wednesday, May 4, 2016

DIWANI KILIMANI AWATAKA WANANCHI WAKE KUJITOKEZA KATIKA UJENZI WA KITUO CHA AFYA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

DIWANI wa kata ya Kilimani katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Simon Ponela amewataka wananchi wake kujitokeza kwa wingi katika ujenzi wa kituo cha afya cha kata hiyo, ikiwemo kuchangia nguvu zao ili ujenzi huo uweze kukamilika kwa wakati.

Oscar Yapesa Mkurugenzi Halmashauri mji wa Mbinga. 
Aidha ujenzi wa kituo hicho ambao hivi sasa umefikia kwenye hatua ya kuweka kenchi kwa ajili ya kuezeka bati, amewataka wananchi hao wajitokeze kuchangia mchanga, tofari na uchanaji wa mbao katika msitu wa kijiji hicho ili ziweze kusaidia katika ukamilishaji wa kazi hiyo ya ujenzi wa kituo cha afya.

Hayo yalisemwa na diwani huyo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, ambaye alitembelea katika kata hiyo kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali za kimaendeleo zinazofanywa na wananchi wa kata hiyo.

Ponela alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho cha afya ulikuwa ukisuasua kutokana na uhaba wa vitendea kazi lakini baada ya yeye kuingilia kati na kuhamasisha wananchi wake na kuushirikisha uongozi wa Halmashauri hiyo kikamilifu, hivi sasa utekelezaji wake unakwenda vizuri ikiwa ni lengo la kuwafanya wananchi waweze kuondokana na kero ya upatikanaji wa matibabu.


“Baada ya kusimama kazi hii ya ujenzi kwa muda mrefu kwa diwani aliyekuwa madarakani wakati huo, mimi nilipochaguliwa mwaka jana nilianza kufanya ufuatiliaji na uhamasishaji juu ya ujenzi wa kituo hiki na wananchi nawashukuru wananiunga mkono na kujitolea kuchangia nguvu zao na halmashauri yetu imekuwa ikitoa vifaa vya kiwandani”, alisema Ponela.

Alisema kutokana na wananchi wa kata hiyo hususani akina mama wajawazito hupata taabu kwa kutembea umbali mrefu kwenda kujifungua hospitali ya wilaya ya Mbinga, ana imani kwamba ujenzi huo utakapokamilika na serikali kuwaletea wahudumu wa afya adha hiyo wanayoipata sasa wataweza kuondokana nayo kutokana na kupata huduma husika kwa karibu zaidi.


Hata hivyo aliongeza kuwa mpaka sasa tayari wananchi wamejitokeza kuchana kenchi 400 za kuezekea kituo hicho cha afya na kwamba ifikapo juni 10 mwaka huu wanatarajia kukamilisha ujenzi huo.

No comments: