Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SERIKALI hapa nchini, imeombwa kufanya jitihada ya kutatua
kero ya uchakavu wa miundombinu ya majengo ya shule ya sekondari Kigonsera
iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ili kuweza kunusuru yasiweze kubomoka
hasa kipindi cha masika ambacho mvua nyingi hunyesha.
Shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1938 hivi sasa miundombinu
mbalimbali kama vile mabweni ya kulala wanafunzi, vyoo na mabafu ya kuogea yana
hali mbaya ambapo yameanza kubomoka kutokana na kutofanyiwa ukarabati kwa muda
mrefu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
Hayo yalisemwa na Emmanuel Sayayi mbele ya mgeni rasmi Mkuu
wa wilaya ya Nyasa, Margaret Malenga ambaye alikuwa akimwakilisha Mkuu wa mkoa
huo Said Mwambungu katika mahafali yao ya wahitimu kidato cha sita
yaliyofanyika shuleni hapo.
Sayayi alisema kuwa shule hiyo ambayo ina historia kwamba
aliyekuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tatu, Benjamin
Mkapa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ni miongoni mwa wanafunzi waliosoma shule
ya sekondari Kigonsera na kwamba, licha ya kuwepo kwa changamoto hizo shule
hiyo pia ina upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi jambo ambalo linasababisha
baadhi yao kutomaliza mihtasari ya masomo kwa wakati.
Alifafanua kuwa serikali iongeze walimu wa masomo hayo,
ikiwemo na zana za kujifunzia vitabu vya ziada, maktaba na vifaa vya maabara
hasa kemikali na gari kwa ajili ya usafiri ili kuweza kutatua changamoto ya
ukosefu wa kukosa kushiriki ziara mbalimbali za kitaaluma, michezo na malezi.
“Tunaiomba pia serikali iingize shule yetu kwenye mpango wa
ruzuku ya mbolea na mbegu za mahindi, ili tuweze kuboresha mradi wetu wa shamba
la mahindi na kadhalika iwekwe kwenye mpango wa kupewa ruzuku ya mafuta ya
kuendeshea jenereta letu au shirika la ugavi wa umeme Tanzania (TANESCO)
lituletee miundombinu ya umeme, tuweze kuondokana na kero ya upatikanaji wa
nishati hii muhimu”, alisema Sayayi.
Pamoja na mambo mengine, akihutubia kwenye mahafali hayo Mkuu
wa wilaya ya Nyasa Margaret Malenga alisema kuwa shule hiyo ambayo inahistoria
nzuri ya kutoa viongozi mashuhuri hapa nchini, hivyo kwa mujibu wa maagizo
yaliyotolewa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Mwambungu, kwamba amemtaka Mkurugenzi
mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo, Venance Mwamengo
ahakikishe anaomba kibali kwa Waziri Mkuu kitakachomfanya aweze kununua gari
jipya na kulikabidhi kwa uongozi wa shule hiyo.
Akizungumzia juu ya suala la upatikanaji umeme shuleni hapo,
amemtaka pia Mkurugenzi huyo kukaa pamoja na Meneja wa TANESCO wa wilaya hiyo
na kuona namna gani wanamaliza kero hiyo ya kupeleka miundombinu ya umeme
shuleni hapo ili wanafunzi hasa wa masomo ya sayansi, waweze kusoma masomo yao
darasani kwa ufanisi mzuri.
Malenga aliongeza kuwa kuhusiana na suala la upungufu wa
walimu wa masomo ya sayansi ameutaka uongozi wa sekta ya elimu mkoani humo,
kuweka kipaumbele katika ajira mpya ya walimu kuhakikisha kwamba walimu
watakaoajiriwa, baadhi yao wapelekwe kwanza katika shule ya sekondari kigonsera
ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo la upungufu wa walimu huku suala la
ukarabati wa majengo ya shule hiyo, alisema atalifikisha kwa uongozi husika
serikalini ili kuweza kuona ni namna gani linapatiwa ufumbuzi wa haraka.
No comments:
Post a Comment