Na Steven Augustino,
Tunduru.
WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti,
yaliyotokea wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, likiwemo la mtu mmoja kuviligwa na
waya wa umeme wakati akipita barabarani.
Zubery Mwombeji. |
Taarifa za matukio hayo zinasema kuwa tukio la kwanza lilitokea
katika msitu wa hifadhi ya Muhuwesi, baada ya mkazi wa kitongoji cha Ngoloanga
kijiji cha Chalinze Kata ya Muhuwesi, Fakii Rashid Mabula (43) alikutwa akiwa
amefariki dunia baada ya kung'atwa na nyoka.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Said Omari Likomanje alisema
kuwa mwili wa marehemu huyo uligundulika Mei 5 mwaka huu baada ya kuripotiwa
kupotea tangu Mei 1 mwaka huu, kwa madai kuwa alikwenda katika msitu huo kwa
ajili ya kutafuta mabanzi ya kujengea zizi lake la mifugo.
Alisema katika tukio hilo mashuhuda hao, walibaini kwamba marehemu
aliumwa na nyoka baada ya kuona kamba ambazo alikuwa amejifunga katika maeneo
mawili ya mguu wake pamoja na meno ya nyoka huyo, jambo lililowafanya wabaini
kuwa kifo chake kilisababishwa na kuzidiwa na sumu ya nyoka huyo.
Kwa mujibu wa taarifa za tukio la pili, ambalo lilitokea
katika eneo la nguzo sita, katika bara bara ya Tunduru kuelekea Songea ambapo
mtu aliyefahamika kwa jina la Yusufu Niiya (32) alifariki dunia baada ya
kuviligwa na waya wa umeme.
Mashuhuda wa tuio hilo walisema kuwa marehemu huyo, alikuwa
anatoka katika eneo la Mwembeliziki kwenda nyumbani kwake eneo la kijiji cha
Nakayaya wilayani humo.
Walisema wakati akiwa njiani, ghafla Lori la mafuta ambalo lilikuwa
likipita bara barani liligonga nguzo na kukata nyaya hizo ambazo zilimuangukia
na kusababisha marehemu kunaswa na umeme, huku dereva aliyekuwa akiliendesha
alilitorosha kwa lengo la kukimbia ili asiweze kupatikana katika eneo hilo la
tukio.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji amethibitisha
kuwepo kwa taarifa hizo na kwamba bado wanaendelea na uchunguzi wa matukio
hayo.
Mwombeji ametoa mwito kwa wananchi wenye taarifa za
kujitosheleza juu ya matukio hayo, walisaidie jeshi hilo kuwanasa mapema
watuhumiwa wa matukio hayo ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria.
No comments:
Post a Comment