Leonidas Gama, Mbunge wa Songea mjini. |
Na Julius Konala,
Songea.
MBUNGE wa jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, Leonidas Gama
amefanya uzinduzi wa tamasha la michezo lijulikanalo kwa jina la Jimbo Cup, ambalo
litashirikisha kata 21 za Manispaa ya Songea mkoani humo.
Uzinduzi huo ulifanyika hivi karibuni kwenye uwanja wa
michezo Majimaji uliopo mjini hapa, ambapo mamia ya wananchi wa Manispaa hiyo waliweza
kushiriki ikiwemo na vikundi mbalimbali vya sanaa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Gama alisema lengo la
kuandaa tamasha hilo ni kwa ajili ya kuimarisha tamaduni za mkoa wa Ruvuma, ikiwemo
hata kuibua na kukuza vipaji vya vijana.
Vilevile alieleza kuwa kupitia tamasha hilo, wataweza kuimarisha
afya zao na kuufanya mji wa Songea kuwa wa michezo pamoja na kuutangaza vivutio
vyake vya utalii.
Mbunge huyo alisema sababu kubwa ya kufanya tamasha hilo ni kuweza
pia kuufanya mji huo, kuwa kisima cha kuzalisha wasanii na wachezaji mbalimbali
wa mpira wa miguu ili timu ya Majimaji iweze kupata wachezaji wenye vipaji.
Amewataka wananchi wa Manispaa hiyo, kujenga ushirikiano katika
kufanikisha jambo hilo kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya.
Kadhalika Gama ameyaomba makampuni mbalimbali, kujitokeza
katika kudhamini mashindano hayo ambayo yanaendelea kufanyika mjini hapa na
kilele chake kitakuwa Mei 7 mwaka huu.
Katika uzinduzi wa tamasha hilo, michezo mbalimbali ilichezwa
ikiwemo kutembea mita 800 kuzunguka uwanja, kuvuta kamba, kufukuza kuku, miziki
ya kizazi kipya ilipigwa, ngoma za utamaduni na mpira wa kengele ambao
ulichezwa na walemavu wa macho (wasioona).
No comments:
Post a Comment