MKuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Na Joyce Joliga,
Songea.
WARATIBU elimu kata katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameshauriwa
kuhakikisha kwamba wanasimamia kikamilifu zoezi la ukusanyaji takwimu kwa
umakini mkubwa ili kuweza kupata usahihi wa takwimu za idadi ya wanafunzi kwa
kila shule za msingi, ziweze kusaidia kuhakikisha vyandarua vinavyogawiwa kwa
wanafunzi hao vinatumika kwa walengwa husika, kwani ikibainika kutoa takwimu za
uongo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Agizo hilo limetolewa juzi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa
hiyo, Jenifer Christian wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja ya
mpango wa ugawaji vyandarua mashuleni, yaliyofanyika mjini hapa.
Hii ni awamu ya nne kwa Waratibu kata, zaidi ya 30 toka
Halmashauri tatu za Manispaa ya Songea, Madaba, pamoja na wilaya ya Songea kupata
vyandarua hivyo ambapo mafunzo hayo yaliandaliwa na shirika lisilo la
kiserikali la PSI.
Alisema kuwa mafunzo hayo yawe msasa na kuwafanya wafanye
kazi kwa weledi mkubwa ili kulifanya zoezi hilo kuwa na mafanikio, ufanisi
mkubwa kwani mpango huo una lengo la kulinda umiliki wa vyandarua katika
ngazi ya kaya ambao umefanikiwa kwa asilimia 85.
Jenifer alisema kuwa katika awamu ya tatu, watoto kuanzia
darasa la kwanza hadi la saba waliweza kupewa vyandarua ambapo jumla ya
vyandarua 494,407 walivigawa katika mikoa mitatu ambapo kwa mkoa wa Ruvuma,
mahitaji yalikuwa vyandarua 188,851.
Mpango huo wa ugawaji wa vyandarua kwa jamii, kupitia watoto hao
waliokuwa katika shule za msingi ni
utaratibu uliobuniwa na serikali kwa kushirikiana na Wizara tatu za Ofisi ya
Rais TAMISEMI, Wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia, wazee na watoto pamoja
na Wizara ya elimu kwa lengo la kuhakikisha jamii inapata vyandarua vya
kutosha na waweze kujikinga na ugonjwa hatari wa malaria.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa PSI mkoa
wa Ruvuma na Njombe Wilfredy Mkungilwa alisema kuwa endapo wanafunzi hao
watapatiwa vyandarua hivyo, kwa kiasi kikubwa itasaidia kupunguza vifo
vinavyotokana na ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment