Tuesday, May 3, 2016

WAKULIMA WA TUMBAKU NAMTUMBO WADAIWA BILIONI 4.2

Na Steven Augustino,
Namtumbo.

IMEELEZWA kuwa vyama vya ushirika 22 ambavyo ni vya wakulima wa zao la tumbaku wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, vinadaiwa shilingi bilioni 4.2 na benki ya CRDB na NMB kutokana na wakulima hao, kushindwa kumaliza kulipa madeni yao katika mikopo waliyokopeshwa na benki hizo kwa lengo la kuboresha kilimo cha zao hilo wilayani humo.

Ofisa kilimo, umwagiliaji na ushirika wilayani humo, Ally Lugendo alisema hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya wakulima hao kwenye mkutano wa wadau wa kufufua zao hilo, uliofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo.
Lugendo alieleza kwamba zao la tumbaku wilayani Namtumbo, limekufa kutokana na wananchi kuacha kulima zao hilo tangu mwaka 2012 huku akibainisha kuwa hilo lilisababishwa na wao kukata tama, kufuatia kutolipwa fedha zao miaka mitatu mfululizo tokea mwaka 2011 hadi 2015.

Alisema kuwa mbali na hilo pia ulimbikizaji wa madeni hayo kwa muda mrefu katika mabenki hayo, ulisababishwa na vyama vya msingi kukopa pembejeo nyingi kuliko hali halisi ya mahitaji ya wakulima na kusababisha madeni kuendelea kukua kwa riba isiyolipika.


Imefafanuliwa pia kitendo cha vyama vya msingi kuchagua viongozi wasio waaminifu na waadilifu, waliandaa makisio zaidi ya mahitaji ya wakulima na matokeo yake wakulima kubeba mzigo mkubwa wa madeni hayo na kukata tamaa ya kuendelea na kilimo cha zao hilo.

Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo,  Asubisye Rajae alisema kuwa kitendo cha wananchi kususia kulima zao la tumbaku kumeisababishia Halmashauri kushuka kimapato, tofauti na ilivyokuwa hapo awali na kwamba wameamua kuanzisha mpango mkakati wa kufufua zao hilo kwa kuwarudisha wananchi shambani huku kukiwa na usimamizi wa hali ya juu unaoendana na kasi ya serikali hii ya awamu ya tano.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Daniel Nyambo pamoja na mambo mengine alizitaka taasisi za kifedha NMB na CRDB kuwapa muda wa miaka mitano kumaliza deni hilo, kwa kulipa kidogo kidogo ili waweze kuzalisha zao hilo kwa wingi.


Wakizungumza kwa niaba ya wakulima wa zao la tumbaku wilayani humo mkulima, Zubery Nchangine na Lucas Ngerangera walifurahishwa na hatua ya Halmashauri yao kuweka mkakati wa kufufua zao hilo, ambalo linategemewa kwa kukuza uchumi wa wilaya hiyo na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

No comments: