Na Muhidin Amri,
Nyasa.
BAADHI ya wajasirimali wadogo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma,
wamesema wanashindwa kujiunga na mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF) na
mfuko wa afya ya jamii (CHF) kutokana na manyanyaso wanayopata wanachama
wa mfuko huo, pale wanapokwenda katika zahanati na vituo vya kutolea
huduma za matibabu wilayani humo.
Walisema kuwa wanapenda kujiunga na mpango huo wa huduma
za afya, NHIF na CHF lakini tatizo kubwa linalowafanya wasite kujiunga na
mifuko hiyo ni pale wanaposhuhudia wenzao ambao tayari wamejiunga, kutopata
matibabu ya haraka kutokana na watoa huduma kwenye vituo hivyo kuwanyanyapaa
kwa madai kwamba wanakosa fedha kutoka kwa watu ambao wanakuja na fedha taslimu
kulipia matibabu.
Walitoa kauli hiyo hivi karibuni, wakati wa zoezi la
uhamasishaji wajasiriamali wadogo ambao ni wateja wa Benki ya Wananchi Mbinga (MCB)
wilayani humo ili waweze kujiunga na mpango huo, ambapo jumla ya wajasirimali
112 waliweza kujitokeza na kujiunga.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake mmoja wa wajasiriamali
hao, Joackim Kamanga alisema watumishi wa afya katika maeneo mengi ya kutolea
huduma za matibabu wilayani Nyasa, wamekuwa na tabia ya kuwanyanyasa na
kuwanyanyapaa wanachama wa mfuko wa afya ya jamii, hatua ambayo inachangia
wananchi wengine kukataa kujiunga na mpango huo.
Kamanga alisema kuwa baadhi ya watumishi hasa wauguzi
wana tabia mbaya ya kuchagua watu wa kuwahudumia kutokana na cheo au nafasi
yake katika jamii, hivyo kukwamisha mpango huo wa serikali wa kuhamasisha
wajasirimali wadogo walioko katika vikundi kuchangamkia fursa ya kujiunga na
mpango huo wa matibabu.
Katika hatua nyingine ameiomba Wizara ya afya,
kuhakikisha kunakuwa na dawa za kutosha kwenye zahanati, vituo vya afya na
hospitali zake ili wananchi waliokubali kujiunga na mfuko wa Taifa wa bima ya
afya na ule wa afya ya jamii waweze kupata huduma bora za matibabu.
Naye Ofisa mikopo wa benki ya wananchi Mbinga, ambao
ndiyo wadhamini wa vikundi hivyo, Pirmin Nchimbi aliwataka wajasiriamali hao
kutokuwa na hofu kuhusu mpango huo badala yake wachangamkie fursa hiyo
iliyotolewa na serikali yenye lengo la kutoa huduma bora za matibabu kwa kila
mtanzania.
Nchimbi aliongeza kuwa benki ya MCB ipo tayari kuhudumia
wateja wake na kwamba ina fedha za kutosha kwa ajili ya kuwakopesha
wajasiriamali wa aina mbalimbali, ili waweze kujiunga na kusonga mbele
kimaendeleo.
Alisema kuwa katika utekelezaji wa mpango huo, benki hiyo
ndiyo itahusika moja kwa moja kuingia mkataba na kulipa michango ya
wajasiriamali wote ambao ni wateja wake, ili nao waweze kuwa sehemu ya
mafanikio ya mpango wa huduma bora za matibabu chini ya mfuko wa Taifa wa bima
ya afya.
No comments:
Post a Comment