Rais John Magufuli. |
Na Muhidin Amri,
Nyasa.
MAISHA ya wavuvi katika mji wa Mbambabay wilaya ya
Nyasa mkoani Ruvuma yako hatarini, kufuatia wavuvi hao kutumia maji ya ziwa Nyasa
ambayo sio safi na salama kwa ajili ya kunywa na matumizi mengine ya kawaida,
katika maisha yao ya kila siku.
Imeelezwa kuwa hali hiyo inatokana na kukosekana kwa
huduma hiyo ya maji katika eneo wanalofanyia shughuli zao za biashara ya
kuuza samaki.
Wavuvi hao pia wameilalamikia Ofisi ya maliasili na
uvuvi wilayani humo kwa kushindwa kupeleka huduma hiyo na miaka mingi sasa
imepita, kwa ajili ya matumizi ya wavuvi na wananchi wengine wanaofika
kwa ajili ya kujipatia kitoweo cha samaki na kufanya shughuli zao za
kujiongezea kipato.
Kutokana na hali hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa
eneo hilo kukumbwa na magonjwa hatari ya mlipuko au kuambukiza kama vile
kuhara, kipindupindu na magonjwa ya matumbo ambayo ni hatari kwa maisha ya
binadamu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wavuvi hao
walisema kuwa, Ofisi husika katika Halmashauri hiyo haina msaada wowote
kwa wavuvi kwani hata pale inapotokea dharura ziwani ya watu kuzama maji,
wao wenyewe ndiyo wanaofanya jitihada ya kujiokoa wenyewe.
Walifafanua kwamba, kila wanapoomba boti ili waweze
kwenda kuwaokoa wenzao hulazimishwa kuweka mafuta kiasi cha lita 30 hadi 50
kwenye boti ya serikali kwa kutumia fedha zao za mfukoni, jambo ambalo limekuwa
ni kero kubwa kwao.
Pia waliongeza kuwa ni haki yao kutumia chombo hicho cha
serikali, lakini ugumu wanaoupata unatokana na watendaji husika kutowajali
wavuvi hao ambao wanamchango mkubwa ndani ya wilaya ya Nyasa.
Kadhalika walisema bado wanakutana na vikwazo
vingi kutoka idara ya uvuvi na maliasili, lakini kinachowasikitisha hasa pale
wanapoona boti hilo hutumika tu kuwasaka wavuvi haramu.
Waliongeza kuwa hata huduma ya choo iliyopo katika eneo
hilo la mwambao wa ziwa Nyasa, imejengwa kwa michango ya wavuvi na
wachuuzi hao ambao walichangishana fedha, baada ya kuona wanapata taabu ya
kupata huduma hiyo muhimu.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mchuuzi wa dagaa
Fatuma Mulemule ameiomba serikali kupitia Waziri mwenye dhamana sekta ya uvuvi
na maliasili kuwachukulia hatua maafisa wao ambao ni kikwazo katika shughuli za
maendeleo ya wananchi.
Mulemule alisema kuwa idara ya uvuvi imekuwa ikihusika
na kukamata mazao ya samaki kutoka kwa wavuvi kwa maelekezo ya Mkurugenzi
mtendaji wa Halmashauri hiyo, Jabir Shekimweri bila kufuata taratibu ikiwemo
pale wanapotoza ushuru wakati mwingine wamekuwa hawatoi stakabadhi halali ya
serikali.
Kwa mujibu wa Mulemule ni kwamba taarifa hizo
wamezikifisha kwa Mkurugenzi huyo, Shekimweri lakini cha kushangaza hakuna
hatua aliyoichukua dhidi ya watumishi wake wanaohusika kufanya hivyo.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa umoja wa wavuvi
wilayani Nyasa Morice Mkinda alisema ni jambo la aibu kuona halmashauri ya
wilaya inashindwa kupeleka huduma ya maji kwenye eneo hilo ambalo linatumiwa
na wavuvi hao, huku wakiendelea kutoza ushuru kila kukicha.
Mkinda alieleza kuwa Mkurugenzi huyo hana ushirikiano na
wavuvi ambapo kila wanapohitaji kukutana naye amekuwa akiwapiga chenga, jambo
linaloonesha kwamba anafanya kazi kwa mazoea hivyo kuna kila sababu kwa Rais
Dkt. John Magufuli kutengua uteuzi wake kwani tayari anaonekana kushindwa
kusimamia kikamilifu maendeleo ya wilaya hiyo.
“Huyu Mkurugenzi ni vyema Mheshimiwa Rais akamuondoa
katika wilaya yetu, huu ni mzigo kweli kweli, hana msaada wowote kwetu ndiyo
maana anashindwa hata kusimamia na kutekeleza majukumu aliyopewa na
viongozi wake wa ngazi ya juu”, alisema Mkinda.
Akijibu tuhuma hizo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo
ambaye pia ni Mhandisi wa maji wa wilaya hiyo, Evaristo Ngole alisema
kuwa matatizo hayo yatafanyiwa kazi na kwamba kuhusiana na tatizo la
upatikanaji wa maji safi na salama katika eneo hilo la wavuvi, wanategemea
kuanza kupeleka huduma hiyo katika eneo hilo baada ya mchakato wa kupata fedha
kwa ajili ya utekelezaji.
“Suala hili la maji kimsingi tunatarajia kuanza kulifanyia
kazi mwezi ujao mara baada ya kukamilika taratibu za kifedha, tayari Ofisi ya
Mkurugenzi imeanzisha mchakato wa kuweza kupata fedha za kujenga miundombinu ya
maji safi na salama, hatutaki wale wenzetu waendelee kutaabika”, alisema Ngole.
Naye afisa maliasili na uvuvi wa wilaya hiyo, Dkt.
Stephen Madondora alikanusha madai ya wavuvi hao kwamba wanawatoza mafuta kwa
ajili ya kwenda kufanya uokoaji pale kunapotokea matatizo ziwani huku akisisitiza
kwamba, wamekuwa wakitoa msaada mara kwa mara kwa wavuvi hao na watu
wengine bila kuwadai chochote.
Madondora alisema serikali tayari imeandaa boti sita
ambazo zitatumika katika ziwa hio upande wa Nyasa, na kwamba pamoja na kufanya
kazi ya doria pia itatumika kwa ajili ya kuokoa wananchi ambao watapata
matatizo wakiwa ndani ya maji.
No comments:
Post a Comment