Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
ZOEZI la uhakiki Watumishi hewa Halmashauri ya wilaya ya
Mbinga mkoani Ruvuma, linaendelea kupamba moto ambapo watumishi 46 ambao
walikwisha staafu wamebainika kuendelea kuchukua mishahara hewa, huku wakijua
kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi.
Rais John Pombe Magufuli. |
Aidha kufuatia msako mkali unaoendelea kufanyika na timu ya
uongozi wa halmashauri hiyo, kati ya hao watumishi 14 wamejisalimisha kituo
kikuu cha Polisi wilayani humo na kwamba wamewekwa mahabusu, kutokana na
kujipatia fedha hizo isivyo halali.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga,
Venance Mwamengo alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake na kuongeza kuwa asilimia kubwa ya waliokamatwa ni wa kutoka
idara ya kilimo na elimu.
Alifafanua kuwa watumishi 24 wameanza kurejesha fedha
walizochukua ambapo hadi kufikia Aprili 28 mwaka huu, jumla ya shilingi milioni
31 zimekusanywa na kurejeshwa hazina.
“Lengo letu ni kuhakikisha kwamba watumishi wote hewa
wanabainika na kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo wote hawa tuliowakamata
na tutakaoendelea kuwakamata watafikishwa Mahakamani ili fedha hizi za wananchi
ziweze kupatikana na kurejeshwa sehemu husika”, alisema Mwamengo.
Alibainisha kuwa uhakiki wa awali waliweza kuwakamata
watumishi hewa 22 na kadiri ya zoezi hilo linavyoendelea kutekelezwa,
walipatikana wengine 24 na kwamba uhakiki huo bado unaendelea.
Pia Mkurugenzi huyo alitoa rai kwa watumishi ambao wanajua
kwamba wamestaafu na bado wanaendelea kuchukua mishahara kila mwezi, wairejeshe
mapema kabla mkono wa sheria haujawafikia.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji
amethibitisha kukamatwa kwa watumishi hao na wengine wakijisalimisha wenyewe
kurejesha fedha za serikali, ambazo walikuwa wakijipatia kwa njia isiyokuwa
halali.
Hata hivyo Mwombeji alieleza kuwa, kwa wale ambao walikamatwa
na kuwekwa mahabusu wapo nje ya dhamana wakati taratibu za kuwafikisha
mahakamani zikiendelea kufanyika.
No comments:
Post a Comment