Wednesday, May 11, 2016

MSUFI WAZUA MAAJABU NAMTUMBO

Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.

MTI aina ya Msufi ambao uliangushwa na Kampuni ya Sogea Satom kupisha ujenzi wa barabara ya lami kutoka Songea kuelekea wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, umezua maajabu na kuwaacha wananchi wa eneo hilo kuishi kwa wasi wasi.

Ujenzi huo wa barabara hiyo ambao ulifanyika mwaka 2014, wananchi wa kijiji cha Nahoro wilayani humo hivi karibuni walifurika katika kijiji hicho kujionea tukio hilo, huku wakiishia kutahamaki na kubaki na mshangao baada ya kujionea mti huo ukiwa umesimama jirani na shimo ulipotolewa.

Omary Kumbakumba mkazi wa kijiji hicho, alisema kuwa hajawahi kuona tukio la aina hiyo ambapo aliwataka wenzake washirikiane naye kuusukuma, ili waweze kuona kama hauanguki.


Katika hali isiyokuwa ya kawaida wananchi waliofika kwenye eneo hilo la tukio, walimtaka kutothubutu kufanya hivyo huku wakidai kuwa jambo hilo linahitaji ujasiri na hakuna mtu aliyejaribu kuungana naye katika wazo hilo la kuusukuma.

Mtendaji  wa kata  ya Luegu wilayani Namtumbo, Zainabu  Maduhu  alithibitisha kusimama  kwa mti  huo katika mazingira  ya kutatanisha  na kusema kwamba baada ya mti huo kuangushwa na kampuni hiyo ya Sogea  ulikuwa  unatumika  kukata  kuni na gogo lake,  lilichanchwa na sehemu ya gogo lililobaki ndilo lililosimama.

Pamoja  na  maelezo  hayo ya mtendaji huyo,  bado sababu za kusimama kwa mti huo zinahusishwa  na imani  za  ushirikina ndio maana wananchi hao walifikia hatua ya kuuogopa na hata kusogea jirani na mti huo.


Pamoja na mambo mengine mti  huo  upo  pembezoni  mwa  bara bara ya  lami  ya  Songea kuelekea Namtumbo,  kijiji cha  Nahoro  katika  kata ya Luegu wilayani humo.

No comments: