Jengo la shule ya msingi Ngapa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, ambalo limeezuliwa kwa mvua iliyoambatana na upepo mkali mwaka 2014. |
Na Steven Augustino,
Tunduru.
WANAFUNZI 589 wanaosoma shule ya msingi Ngapa, wilayani
Tunduru mkoa wa Ruvuma wapo katika hatari ya kufanya vibaya katika masomo yao,
kutokana na shule hiyo kubomoka na kukosa mahali pa kusomea masomo yao.
Hali hiyo inawafanya wanafunzi hao, kusoma kwa kupeana zamu
katika madarasa matatu kati ya saba yanayohitajika wakati wanapokuwa katika
vipindi vyao vya masomo darasani.
Jengo ambalo limeezekwa kwa nyasi wanalotumia sasa kusomea. |
Tatizo hilo limedumu kwa muda mrefu na kusababisha madarasa
manne yaliyopo katika shule hiyo kubomolewa na mvua ya mawe, ambayo iliambatana
na upepo mkali Februari 5 mwaka 2014.
Aidha taarifa za awali zinaeleza kuwa, sambamba na kubomolewa
kwa madarasa hayo shule hiyo haina hata vyoo vya kujisaidia wanafunzi hao jambo
ambalo linawafanya wajisaidie porini kipindi chote tangu mwaka huo, shule hiyo
ilipokumbwa na mkasa huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wazazi na walezi wa watoto
hao walisema kuwa, kinacho washangaza ni kwamba tangu wakati huo hawajawahi
kuwaona viongozi ngazi ya serikali, kwenda kutoa msaada waina yoyote au kufanya
jitihada juu ya ujenzi wa vyoo na madarasa hayo yaliyobomoka.
Wananchi hao waliiomba serikali, kupitia Wizara ya
elimu kuingilia kati na kuhakikisha shule hiyo inajengwa ili kuwawezesha
watoto hao kusoma katika mazingira mazuri.
Katika tukio hilo walisema, pia mvua hiyo ilibomoa nyumba 36 za
wananchi waishio karibu na shule ya msingi Ngaga na kuwaacha wakazi wake,
wakiwa hawana mahali pa kuishi.
Mwalimu Mkuu shule hiyo, Christopher Mnipa alithibitisha
kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kwamba kuna kila sababu kwa serikali kuchukua
hatua za haraka ili kuweza kunusuru hali hiyo.
Tina Sekambo ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya ya Tunduru pamoja na kukiri kuwepo kwa tatizo hilo, alisema kwamba kilichowafanya
washindwe kutekeleza ujenzi wa madarasa hayo kinatokana na wananchi kukataa
kujitolea kuchangia nguvu zao ili ujenzi uweze kuanza mara moja.
Hata hivyo, alisema Halmashauri hiyo kwa kushirikisha wataalamu wake wanajipanga kwenda kutoa elimu na hamasa kwa wananchi hao kujitokeza kuchangia nguvu zao na halmashauri, iweze kununua vifaa vya ujenzi ili kuweza kumaliza tatizo hilo ambalo limedumu kwa muda mrefu sasa.
No comments:
Post a Comment