Na Steven Augustino,
Tunduru.
WATU watatu wamelazwa katika hospitali ya Misheni ya Mbesa wilayani
Tunduru mkoani Ruvuma, baada ya kujeruhiwa na mamba katika matukio tofauti
yaliyojitokeza wilayani humo.
Hayo yamebainishwa na Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dokta
Ires Sekreman wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu katika mahojiano
yaliyofanyika kwa njia ya simu, ambapo pamoja na mambo mengine hospitali hiyo
ambayo ipo pembezoni mwa Tanzania imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi hao, ambao
hukumbwa na matatizo ya aina mbalimbali ya kiafya.
Dokta Sekreman alisema kwamba amekuwa akipokea majeruhi na
wagonjwa wengi kutoka katika vijiji vilivyopo nchi jirani ya Msumbiji hasa
ambao hujeruhiwa na mamba, ambayo huwapata wakati wakivua samaki na kufanya
shughuli hizo katika mto Ruvuma.
Alimtaja majeruhi wa kwanza kuwa ni, Addo Adam (29) mkazi wa
kijiji cha Kazamoyo tarafa ya Lukumbule wilayani Tunduru ambapo kutokana na
hali aliyokuwa nayo majeruhi huyo, maafisa tabibu na wataalamu wa hospitali
hiyo ya Mbesa walikubaliana kumkata mguu wake wa kulia ili kuokoa maisha
yake kutokana na kuharibiwa vibaya.
Alisema majeruhi huyo ambaye alipokelewa April 16 mwaka huu,
mguu huo uliharibika vibaya baada ya kutafunwa na mamba huyo na kwamba endapo
kama usingekatwa ungeoza na kumfanya apoteze maisha.
Kadhalika alimtaja majeruhi mwingine kuwa ni Sharif Makunga
ambaye pia alikuwa akipatiwa huduma ya matibabu katika hospitali hiyo, kutokana
na kujeruhiwa na mamba.
Akizungumzia matukio hayo kaimu Afisa wanyamapori wilayani Tunduru,
Peter Mtani pamoja na kuthibitisha uwepo wa matukio hayo alifafanua kuwa katika
kipindi hicho, Zainabu Kopwe aliuawa na mamba katika mto huo wakati akiwa
anaoga ambapo tukio hilo lilitokea March 18 mwaka huu.
Mtani alisema kuwa chanzo cha matukio hayo, kinatokana na
jamii wakati wote katika uwanda huo wa mto Ruvuma hutegemea maji ya mto huo kwa
shughuli mbalimbali.
Alisema katika matukio yote yaliyoripotiwa na ambayo mengine
idara yake haikuyapata huwatokea hasa wakiwa wanaoga, kuchota maji kwa ajili ya
kunywa na kufulia nguo zao, huku wengine hupatwa na mikasa hiyo pale
wanapokwenda kuvua samaki kwenye mto huo.
Hata hivyo alisema suluhisho kubwa namna ya kuwaepusha watu
hao ili waweze kuepukana na matatizo hayo, kuna kila sababu kwa serikali
kufanya jitihada ya kuwapelekea maji safi na salama ya bomba au kisima, ili
waweze kuepukana na kadhia hiyo wanayoendelea kuteseka nayo kwa muda mrefu
sasa.
No comments:
Post a Comment