Betramu Sanga ambaye ni afisa kilimo (katikati) akiwapa maelekezo juu ya kilimo bora cha zao la mpunga wakulima wa kijiji cha Mabuni kata ya Litumbandyosi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAKULIMA wanaozalisha zao la mpunga katika mradi wa
umwagiliaji Sanga mabuni uliopo kijiji cha Mabuni kata ya Litumbandyosi wilaya
ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba Halmashauri ya wilaya hiyo kufanya jitihada
ya kukamilisha ujenzi wa mfereji wa kuleta maji shambani ili waweze kuzalisha
zao hilo kwa wingi.
Aidha wameeleza kuwa mfereji huo unaoleta maji shambani ambao
una urefu wa mita 5,850 kutoka kwenye banio kuu la umwagiliaji, ambapo
zilizojengwa mpaka sasa ni mita 3,175 na kwamba zilizobakia ni mita 2,625
ambazo bado ujenzi wake haujakamilika na kuweza kuleta maji kwenye mashamba
yaliyopandwa zao hilo.
Silvester Ngonyani ambaye ni Mwenyekiti wa mradi huo, alisema
hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea kwa lengo
la kujionea mafanikio wanayoyapata na changamoto mbalimbali ambazo hukabiliana
nazo wakulima hao.
“Hivi sasa kama mfereji huu ungekamilika ujenzi wake malengo
yetu ni kuzalisha zaidi ya gunia 40 za mpunga, lakini tunashindwa kufikia lengo
hili kutokana na mfereji huu kutokamilika ujenzi na kuweza kuleta maji mengi
shambani”, alisema Ngonyani.
Ngonyani alifafanua kuwa wanaiomba pia serikali iwatazame kwa
jicho la huruma wakulima wanaozalisha zao la mpunga kwa kuwapatia ruzuku ya
pembejeo za kilimo ili waweze kuzalisha mpunga kwa wingi na kuweza kuondokana
na umaskini miongoni mwao.
Alisema kuwa mradi wa umwagiliaji Sanga mabuni umesajiliwa
kisheria na kwamba ulianza kazi rasmi ya umwagiliaji mwaka 2004, hivi sasa una
wanachama 122 wakiwemo wanawake 61 na wanaume 61 ambao hufanya kazi ya
kuzalisha zao la mpunga kwa njia ya umwagiliaji.
Theresia Kinyeru ambaye naye ni mkulima na mwanachama katika
mradi huo, alitoa ushauri wake akisema kwamba ili waweze kuondokana na kero
hiyo ya upatikanaji wa maji, ni vyema serikali ikaweka mpango wa kuwajengea
bwawa kubwa la kuhifadhia maji ambalo katika kipindi cha mwaka mzima wataweza
maji hayo kuyatumia katika shughuli za umwagiliaji.
Kinyeru alisema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto hizo,
lakini wanaushukuru uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kwa kuwajengea
mradi huo ambao umekuwa ni msaada mkubwa kwao, wameweza kuwa na kipato kwa
kujenga nyumba za kisasa ambazo zimeezekwa bati.
No comments:
Post a Comment