Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, imepokea vifaa
vya michezo mpira wa miguu na pete kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini,
Sixtus Mapunda ili viweze kusaidia vijana wanaotoka katika baadhi ya shule za
sekondari zilizopo katika mji huo, kushiriki kikamilifu mashindano ya Umoja wa
Michezo Sekondari Tanzania (UMISETA) ngazi ya wilaya na mkoa.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa mji huo, Oscar
Yapesa ambavyo ni jezi zenye thamani ya shilingi 650,000 kwa niaba ya Mbunge
huyo, Geddy Ndimbo ambaye ni katibu wake alisema kuwa wawakilishi wa timu ya
Kombaini ya vijana wa shule hizo, ndio watakaoshiriki mashindano hayo ambayo
yanatarajia kuanza kutimua vumbi Juni 2 Mwaka huu katika uwanja wa michezo
wa shule ya sekondari Makita uliopo mjini hapa.
Geddy alifafanua kuwa ufadhili huo uliotolewa na Mbunge
Mapunda ni endelevu na kwamba lengo ni kutafuta vijana watakaoweza kuunda timu
ya mkoa huo, ambao baadaye wataungana na wenzao wa kutoka katika maeneo
mbalimbali ndani ya mkoa.
“Idara ya Ofisa utamaduni na michezo pia na elimu ya
sekondari tunaipongeza kwa maandalizi inayoyafanya katika kushiriki kikamilifu
kwenye mashindano haya, ambayo yataweza kukuza na kuendeleza vipaji kwa vijana
wetu”, alisema Geddy.
Alisema kuwa timu hiyo ya Kombaini ya kutoka hapa Mbinga, anapenda
kuona inaendelea kufanya vizuri hadi ngazi ya mkoa ili pia iweze kusonga mbele
zaidi.
Katibu huyo wa Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini aliongeza kuwa
mpango alionao Mbunge Mapunda kwa siku za usoni, anahitaji kuwekeza katika
sekta ya michezo kwa vijana wa shule zote za sekondari zilizopo katika jimbo
hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji huo, Yapesa alishukuru
msaada huo uliotolewa na Mbunge huyo ambao unalenga kuwasaidia vijana hao,
waweze kufanya vizuri katika sekta ya michezo na kukuza vipaji vyao.
No comments:
Post a Comment