Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WILAYA ya Mbinga mkoani Ruvuma, imetenga zaidi ya shilingi
milioni 475.8 kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa madawati, meza na
viti kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ikiwa ni utekelezaji
wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli, alilotoa hivi karibuni wakati
akiwaapisha wakuu wa mikoa na kuzitaka halmashauri zote hapa nchini
kuhakikisha zinamaliza tatizo hilo.
Aidha wilaya hiyo tayari imefanikiwa kutengeneza madawati 6,134
kati ya madawati 12,952 ambapo kwa shule za msingi madawati yaliyokamilika ni 3,634
na shule za sekondari 2,500 sawa na asilimia 47.6 ya lengo kwa gharama ya
shilingi milioni 169 na tayari yamekwisha sambazwa kwenye shule husika, huku
mchakato wa kumaliza madawati 5,510 kwa shule za msingi 3,810 na sekondari 1,700
ukiwa katika hatua ya mwisho kukamilika kwake.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya ya Mbinga vijijini, Venance Mwamengo wakati alipokuwa akitoa
taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa, George Mbijima
katika kijiji cha Mbuji kata ya Mbuji wilayani humo.
Kwa mujibu wa Mwamengo alieleza kuwa kiasi hicho cha fedha ni
gharama za kununulia mashine za kuranda, kukata na kukunja vyuma, mashine za
kupasulia mbao, umeme na gharama zingine ndogo ndogo na kwamba madawati hayo yametengenezwa
kwa kutumia mbao pamoja na chuma ili yaweze kuwa imara tofauti na madawati
yanayotengenezwa kwa mbao tupu, ambayo huharibika kwa haraka na hayadumu kwa muda
mrefu.
Mwamengo alisema kuwa wilaya hiyo yenye halmashauri mbili ya
Mbinga mjini na Mbinga vijijini ilikuwa na upungufu wa madawati 12,952
ambayo katika shule za msingi upungufu ulikuwa madawati 8,452 viti na meza kwa
shule za sekondari upungufu ulikuwa 4,500 ambapo katika utekelezaji wa agizo la
serikali walianza kutengeneza madawati mwezi Januari mwaka huu na kwamba wanatarajia
kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Alisema kuwa mradi wa kutengeneza madawati ya wanafunzi wa
shule za msingi na sekondari, ulianzishwa ili kutekeleza agizo la serikali ya
awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika kuhakikisha kwamba
halmashauri zinapunguza kero hiyo ya upungufu wa madawati, ili kuweka mazingira
mazuri ya kusomea wanafunzi na walimu kufundisha watoto wanapokuwa darasani.
Kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa
George Mbijima, amewapongeza viongozi wa wilaya hiyo kutokana na jitihada
wanazozifanya pamoja na ubunifu wa miradi mingi na mizuri ya maendeleo ya
wananchi, ambayo imejengwa kulingana na thamani halisi ya fedha.
Mbijima amewataka wananchi, watumishi na viongozi wa serikali
wilayani Mbinga, kutobweteka na mafanikio waliyonayo badala yake waongeze juhudi
katika kufanya kazi na viongozi kutumia muda mwingi kutatua matatizo
yanayowakabili wananchi.
Katika hatua nyingine aliwaagiza wahakikishe pia wanashirikisha
makundi ya vijana katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Wapeni kipaumbele vijana ili nao waweze kutambua wajibu wao,
mkifanya hivi ni hatua nzuri itakayosaidia kuongeza juhudi katika kukabiliana
na changamoto zinazowakabili, kama vile ukosefu mitaji kwa ajili ya
kuanzisha miradi ya kiuchumi”, alisema Mbijima.
Vilevile kiongozi huyo wa mbio za Mwenge kitaifa, amewataka
wazazi na walezi wilayani humo kushirikiana na serikali katika kutatua tatizo
la upungufu wa madawati kwa shule za msingi na sekondari, ili kuwawekea
mazingira mazuri watoto wao wanapokuwa darasani waweze kupenda kusoma na kufanya
vizuri katika mitihani yao.
Pia ameviagiza vyombo vya dola kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani
wanaume wenye tabia ya kuwarubuni wasichana ambao bado wanasoma shuleni kwa
kufanya nao mapenzi, kwa sababu wamekuwa chanzo kwa wasichana wengi hapa nchini
kukatisha masomo yao.
No comments:
Post a Comment