Na Kassian
Nyandindi,
Namtumbo.
WILAYA ya Namtumbo na vitongoji vyake mkoani Ruvuma,
inakabiliwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama jambo ambalo
linasababisha wananchi wake washindwe kuendesha shughuli zao za kiuchumi
ipasavyo, katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya wilaya hiyo.
Aidha imeelezwa kuwa hali hiyo inachangiwa na baadhi ya
wananchi, kuharibu vyanzo vya maji kutokana na kukata miti hovyo na kuendesha
shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo hivyo.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Ali Mpenye
alisema hayo leo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili ya mradi wa athari
na changamoto za madiliko ya tabia nchi kwa wanawake wa wilaya hiyo, ambayo
yamefadhiliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Women Fund Tanzania (WFT) yaliyofanyika
kwenye ukumbi wa Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Namtumbo mjini hapa.
Mpenye alisema kuwa wilaya hiyo ambayo ina idadi ya watu
214,000 sehemu kubwa ya wananchi wake, wamekuwa wakijishughulisha na shughuli
za kilimo katika vyanzo vya maji kitendo ambacho kinasababisha vianze kukauka
na kupoteza uoto wake wa asili.
“Wale wote ambao wanafanya shughuli za kibinadamu kwenye
vyanzo vya maji, tunawataka waondoke, kwa sababu wanaharibu mazingira na
kutishia usalama wa maendeleo ya viumbe hai ikiwemo sisi wenyewe binadamu”,
alisema Mpenye.
Alisema kuwa serikali itaendelea kuwachukulia hatua watu
wanaoharibu mazingira ambapo katika wilaya ya Namtumbo, tayari kuna barua za
onyo zimesambazwa kwenye maeneo husika kwa ajili ya kuwataka watu waondoke
kwenye vyanzo hivyo.
Vilevile aliwataka wanawake wilayani humo ambao wanashiriki mafunzo
hayo kuwa mstari wa mbele, kuelimisha jamii iachane na shughuli zinazochangia
uharibifu wa mazingira.
“Tatizo hili ni kubwa, lakini watu bado ni wabishi wanataka
waendelee kulima mashamba yao katika vyanzo vya maji ninyi akina mama mnatakiwa
muwe mabalozi wazuri wa kukemea hali hii kwa nguvu zote ili tuweze kuwa na maji
ya kutosha ya kuendeshea shughuli zetu kiuchumi”, alisema.
Awali kwa upande wake, Terdey Mhagama Mkurugenzi mtendaji wa
shirika la MWECO lisilokuwa la kiserikali hapa nchini, ambalo linajishughulisha
na kujenga uwezo wa masuala ya kiuchumi kwa jamii hususani wanawake katika
upatikanaji wa rasilimali za maji, uhifadhi wa vyanzo vya maji na mazingira
alisema kuwa mabadiliko hayo ya tabia nchi husababisha madhara makubwa kwa
jamii na hata kuathiri kizazi cha sasa na baadaye.
Mhagama alieleza kuwa ni takribani miongo mitatu sasa, dunia
imekuwa ikikabiliwa na majanga anuwai ambayo husababisha hasara kubwa na
upotevu wa mali na maisha ya watu, hivyo kuongezeka kasi ya watu kuathirika
kiuchumi na kuwa maskini.
“Kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu kunaathiri mfumo mzima
wa hali ya hewa na mazingira kama vile ukataji wa miti hovyo, uvuvi mkubwa baharini
usiozingatia utaalamu, uanzishwaji wa viwanda vikubwa vya kemikali na madini na
matumizi mabaya ya ardhi kunasababisha mabadiliko ya tabia nchi”, alisema
Mhagama.
Alisema kuwa hali hiyo inapojitokeza waathirika wakubwa ni
wanawake ambao hupoteza muda mwingi kutafuta maji, na hivyo kuathiri
utekelezaji wa shughuli zingine za kujipatia kipato na kujiletea maendeleo.
Pamoja na mambo mengine alibainisha kuwa katika nchi za
Afrika, Tanzania ni nchi ambayo inaathirika zaidi na athari za mabadiliko ya
tabia nchi ukizingatia kwamba ni wachangiaji wadogo wa tatizo hilo, hivyo kuna
kila sababu kuwa mstari wa mbele kukemea hali hiyo kwa kuzitaka nchi zinazoongoza
kuleta mabadiliko hayo, kupunguza madhara ili jamii isiweze kuathirika.
Hata hivyo kusudio la mradi huo wilayani Namtumbo, ni pamoja
na kuunda mtandao wa wanawake katika eneo lililokusudiwa kwa kuwajengea uwezo
na kushawishi kuongea kwa kupaza sauti zao katika kukabiliana na mabadiliko ya
tabia nchi, sanjari na kuendesha mdahalo wa pamoja kati ya wanawake na wadau
wengine.
No comments:
Post a Comment